Mwanafunzi anusurika kipigo akidaiwa kujifungua, kutupa mtoto

Muktasari:

  •  Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (Saut) Mwanza aliyetambulika kwa jina moja la Judith amenusurika kipigo kutoka kwa wananchi  akidaiwa kujifungua na kumtupa mtoto nyuma ya nyumba anayoishi.


Mwanza. Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (Saut) Mwanza aliyetambulika kwa jina moja la Judith amenusurika kipigo kutoka kwa wananchi  akidaiwa kujifungua na kumtupa mtoto nyuma ya nyumba anayoishi.

Mwanafunzi huyo anayesoma shahada ya sheria mwaka wa tatu chuoni hapo anadaiwa kutenda tukio hilo leo asubuhi Jumatatu Juni 20, 2022 nyumbani kwake mtaa wa Silivin Sweya jijini Mwanza.

Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Silivini, Rajabu Ramadhan amethibitisha kutokea tukio hilo akibainisha kuwa mtuhumiwa yupo chini ya ulinzi wa polisi.

"Baada ya kukuta mwili wa kichanga umetupwa tulifanya msako wa kujua mtu aliyekuwa na ujauzito na tulimbaini mwanafunzi wa Saut ambaye baada ya kumchunguza tumekuta ana dalili za kutoa mimba kwani alikuwa akitokwa na damu," amesema Ramadhani

Kwa upande wake, waziri wa ulinzi wa serikali ya wanafunzi chuoni hapo, John Matemba amekiri mwanafunzi huyo kusoma chuoni hapo huku akilaani kitendo hicho kwamba serikali ya wanafunzi  imekuwa ikitoa elimu ya uzazi kwa wanafunzi mara kwa mara.

"Tulitoa elimu wanapokuwa wamepata ujauzito jinsi gani wanatakiwa kufanya, kama wameshindwa kuhimiri wanatakiwa wafike kwenye ofisi ya mlezi wa chuo wapaye ushauri lakini tunashangaa kuona mtu anafanya kitu cha namna hii," amesema Matemba

Shuhuda wa tukio hilo, Felister Severine amesema amebaini kuwepo tukio hilo baada kusikia kelele za mtuhumiwa akilalamika kupata maumivu ya tumbo jambo lililomfanya atoke nje na kukutana na matone ya damu yaliyoanzia katika mlango wa chumba cha mtuhumiwa hadi nje ya geti.

 "Tulipotoka nje baada ya kusikia kelele tulikutana na matone kuanzia kwenye chumba chake hadi nje ya geti kufuatilia damu hiyo ndipo tukakutana na kichanga kilichokufa kikiwa kimetelekezwa nje ya geti," amesema Felister

Mkazi wa mtaa wa Silivini, Gabriel Augustino amesema tukio hilo ni mwendelezo wa matukio ya wanafunzi kutoa mimba na kutelekeza vichanga akidai kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu katika mtaa huo kumeripotiwa matukio matatu ya vichanga kutupwa.

"Wanawake hasa wanafunzi wanaoishi katika eneo hili, wakipata ujauzito wasijione wa tofauti badala yake waichukulie kama hali ya kawaida. Kutoa mimba siyo utatuzi wa tatizo bali kuteketeza kizazi kijacho," amesema Augustino.