Mwanafunzi aolewa kwa Sh30,000, DC aingilia kati

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro

Muktasari:

  • Njama za Mohamed Salum kumuoa mwanafunzi aliyekuwa akitarajiwa kuijiunga na kidato cha tano mwaka huu zimezimwa baada ya kushtukiwa na Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro.

Tunduru. Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro amefanikisha kuvunja ndoa ya kimila iliyokuwa imefungwa baina ya muuza urembo, Mohamed Salum, na mwanafunzi wa kidato cha tano kwa mahari ya Sh30,000.

Tukio hilo lilitokea jana Alhamis usiku kwenye Kijiji cha Muungano, Tunduru Mjini wilayani humo ambapo mtuhumiwa alikuwa akiishi na mwanafunzi huyo.

Binti huyo wa miaka 20, alikuwa amechaguliwa kujiunga na elimu ya kidato cha tano katika Shule ya Wasichana ya Masasi na ilikuwa aanze masomo yake Agosti mwaka huu.


Katika tukio hilo Mtatiro aliyekuwa ameongozana na vyombo vya usalama alimkamata mtuhumiwa aliyemuoa mwanafunzi huyo, baba wa binti huyo, Othuman Ally na washenga wake.

Akieleza walivyoweza kuoana na binti huyo baada ya kuhojiwa, Mohammed alisema kabla ya kufanya maamuzi hayo alimuuliza msichana kama amemaliza shule na kumuhakikishia hilo na kumeleza kuwa hana uhakika kama ataendelea.

“Aliniambia amemaliza shule lakini hana uhakika hata akifaulu kama ataendelea, hivyo nikamwambia ngoja niandike barua ili tukae sehemu moja tuanzishe maisha pamoja.

“Nikatafuta kwanza hela Sh50,000 kwa ajili ya barua halafu nikakaa tena siku nyingine nikapeleka Sh30,000 ya kukalisha na mzazi wake alinuruhusu nimuoe,”amesema Salum.

Kwa upande wake baba mzazi wa binti, Othuman Ally amekiri kumuoza mtoto wake huyo kwa mahari ya Sh30,000 kwa madai kuwa binti hakuwa tayari kuendelea na kidato cha tano.

“Mimi nilishtukia mtu kaja hapa kuleta barua na hata nilipomuuliza mtoto vipi kuhusu shule alisema hataki kuendelea na kama nitamlazimisha atajishikisha mimba ili asiendelee na masomo,”alisema Ally.

Hata hivyo, DC Mtatiro alivyomuhoji binti huyo kama anataka shule au la alisema ataendelea ikiwa atapewa nafasi hiyo.

Mtatiro amesisitiza binti huyo atasimamiwa aendelee na masomo yake na kuendeleza ndoto yake.

Pia alitumia nafasi hiyo kuwaasa wazazi wa Tunduru kuachana na mambo ya kizamani ya kuoza mabinti ambao wana nafasi ya kuwa na mchango mkubwa zaidi kwa taifa.

“Matukio ya mabinti wa shule kuozesha hapa Tunduru yamekuwa mengi lakini ugumu tunaoupata katika kuushughulikia ni wazazi kula njama za kuwatorosha mabinti wao pale wanapojua wanafuatilia ili wasikamatwe,”amesema Mtatiro.