Mwanafunzi chuo cha Mtakatifu Joseph auawa kwa kuchomwa kisu

Hajrat Shaban (22), Mwanafunzi wa Chuo cha Mtakatifu, Joseph kilichopo Mkundi, Morogoro  aliyeuawa baada ya kuchomwa kisu na watu wasiofahamika, baada ya kuvamiwa usiku wa Aprili 16,2024  Picha na Johnson James

Muktasari:

  •  Mwanafunzi huyo ameuawa Jumanne Aprili 16, 2024 baada ya kuchomwa kisu na kusababisha atokwe na damu nyingi.

Morogoro. Mwananfunzi wa Chuo cha Mtakatifu Joseph cha mkoani hapa ameuawa kwa kuchomwa kisu na mtu asiyejulikana.

Mwanafunzi huyo aliyejulikana kwa jina la Hajrat Shaban (22), anadaiwa kuuawa baada ya kuvamiwa akiwa hosteli za chuo hicho zilizopo eneo la Mkundi mkoani Morogoro.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Aprili 17, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amethibitisha  kutokea kwa tukio hilo.


Askari Polisi Kata ya Mkundi, Manispaa ya Morogoro akizungumza na wanafunzi wa Chuo cha Mtakatifu Joseph baada ya mwanafunzi mwenzao kuuawa na mtu ambaye hajafahamika nje ya hosteli waliyokuwa wakiishi. Picha na Johnson James


Amesema mwanafunzi huyo ameuawa jana Jumanne Aprili 16, 2024 na muuaji alimchoma na kisu na kusababisha atokwe na damu nyingi iliyosababisha mauti yake.

“Tunafanya uchunguzi wa mauaji ya Hajrat Shaban, huyu ni mwanafunzi wa Chuo cha Mtakatifu Joseph kilichopo Mtaa wa Bwawani na tukio hilo lilitokea saa 2:00 usiku,” amesema kamanda huyo.

Akisimulia tukio hilo, Kamanda Mkama amesema Hajrat na wenzake walikuwa wanajaribu kumdhibiti kijana aliyeingia kwenye hosteli zao kwa lengo la kuiba simu.

Amesema katika purukushani ndipo kijana huyo akachomoa kisu na kumchoma binti huyo.

“Na alipopelekwa zahanati iliyoko jirani na maeneo yale iitwayo Habemes kwa matibabu, Hajrat akawa ameshafariki dunia,” amesema kamanda huyo.

Ametoa wito kwa wenye nyumba za biashara na makazi kuhakikisha kunakuwa na ulinzi mara zote ili kuwahakikishia usalama wapangaji wao.

“Hakuna mtu tunayemshikilia mpaka sasa kuhusu tukio hilo,” amesema kamanda huyo.


Wenzake wazungumza

Amos Dimata, rais wa serikali ya wanafunzi chuoni hapo, amesema wakati tukio linatokea alikuwepo katika hosteli hizo, alikofika baada ya kuitwa na wenzake akasikilize malalamiko yao.

 “Wenzangu waliniita nije kuzungumza nao, baada ya mazungumzo mimi na wenzangu tukatoka nje huku tukiagana nao, Hajrat alinifuata akitaka nimsaidie kurekebisha kitu kwenye simu yake, ndipo akatokea huyo jamaa akataka kukwapua ile simu,” anasimulia Dimata.

Amesema mtu huyo alipoona anazidiwa, akachomoa kisu na kuanza kumchoma nacho yeye mkononi, kabla ya kumchoma Hajrat mkononi, shingoni na mgongoni na kisha akatokomea.

“Tukio hili ni kubwa, nadhani vyombo vya ulinzi na usalama vinapaswa kuchukua hatua, ukiangalia eneo hili halipo kwenye mazingira salama, mtu akiamua kufanya tukio lolote usiku anaweza, tena bila kukamatwa,” amesema.

Rais huyo amesema hata vituo vya polisi haviko jirani, viko mbali na maeneo hayo, jambo linalotoa mwanya kwa wahalifu kufanya bila kuwa na hofu ya kukamatwa.

Dimata amesema wamepoteza nguvu kazi ya Taifa kwa sababu Hajrat alikuwa mwanafunzi aliyekuwa akisoma masomo ya biashara na alikuwa mwaka wa tatu akiwa ukingoni kuhitimu.

Naye Imaleda Dokta rafiki wa marehemu amesema tukio hilo lilitokea wakati wanahamishwa kutoka hosteli hiyo kwenda hosteli nyingine.

“Tulikuwa ndani tunakula, walimu wakaja kutaka kutuhamisha kwenda hosteli nyingine, hatukutaka, ndipo tukawaita viongozi wetu waje kutusikiliza.

“Sasa wakati viongozi wa serikali ya wanafunzi wanajadiliana, Hajrat alikuwa ndani na wenzake waliokuwa wanakula, baadaye akatoka nje ya geti ili akazungumze na rais wa chuo amtengenezee simu yake iliyokuwa inamsumbua upande wa intaneti, hapo ndipo yalipotokea hayo yote,” anasema Dokta.

Anasema mtu huyo ambaye alikuwa na wenzake waliokuwa na bodaboda walitokomea kusikojulikana baada ya wanafunzi kupiga kelele za mwizi.

Mkuu wa chuo hicho, Julius Usiga amesema taarifa za kuuawa kwa Hajrat alizipata saa mbili usiku.

“Nilipata taarifa kwamba mwanafunzi wetu Hajrat Shaban ameuawa kwa kuchomwa kisu sehemu tatu za mwili wake na vijana wawili waliofika kwa bodaboda eneo la hosteli,” amesema.

Hata hivyo, amesema matukio ya watu kuvamiwa katika eneo hilo yapo mara nyingi na hivyo ametoa rai kwa mamlaka zinazohusika kuchukua hatua.

Anasema Desemba 2023, kundi la watu lilivamiwa eneo hilo likavunja na kuiba kwenye nyumba za watu na hakuna mtu aliyekamatwa.

Akizungumzia malalamiko ya wanafunzi juu ya usalama wao, mkuu huyo wa chuo amesema wana utaratibu wa kubadilisha walinzi kila mara kwa lengo la kuimarisha ulinzi.

“Na tukipata changamoto kama hivi huwa tunatoa taarifa polisi watusaidie kuimarisha ulizi,” amesema mkuu huyo wa chuo.

Mwenyekiti wa mtaa huo, Zainabu Risasi ambaye pia hupika chakula na kuwauzia wanafunzi hao, amesema:

“Jana usiku nilikuwa nimekaa nyumbani kwangu nikasikia kelele za mwizi, nikamwambia mwanangu huko wanaitia mwizi inawezekana hii bodaboda ambayo imepita hapa ndiyo imeleta balaa huko tuikamate lakini hatukuwahi.”

Amesema hali ya usalama katika eneo hilo si nzuri kwa kuwa wanafunzi wanaoishi kwenye hosteli hizo huvamiwa mara kwa mara na vibaka na kuporwa vitu vyao.

“Ili uvamizi wa safari hii umekuwa mkubwa, huwa watoto wanaibiwa simu, hela au mabegi ya kompyuta ila hakujawahi kutokea mauaji,” amesema mwenyekiti huyo.

Ametoa rai kwa uongozi wa chuo kuongeza ulinzi kwenye hosteli hizo anazozema zinakaliwa zaidi na watoto wa kike.

Zabron Philemon, mkazi wa eneo hilo anaungana na mwenyekiti akisema wimbi la vibaka ni kubwa eneo hilo na hawawaibii wnafunzi pekee, bali hata wakazi wa maeneo hayo ya Bwawani.

“Kero hii ni ya muda mrefu sasa kwenye huu mtaa wetu, vibaka ni wengi lakini hata mazingira ya eneo hili si salama, kuna pori kubwa, uongozi wa chuo utafute eneo lingine ambalo ni salama kwa vijana wetu, huku hapana,” amesema Philemon.

Mkazi mwingine wa Bwawani, Samora James anasema changamoto ya mtaa huo ni wizi na vibaka aliodai wanatokea eneo la mizani ya zamani.

“Eneo hili lina uhalifu wa kutosha, watu wanaporwa simu kila siku, na hao vibaka wakishapora hukimbilia kule kwenye makaburi wanajua hakuna mtu anaweza kuwafuata kwa sababu kuna pori,” amesema.

Patrick Lumata, mwenyekiti Mtaa wa Bwawani Kata ya Mkundi anakiri eneo hilo kuwa na vibaka wanaowasumbua wanafunzi mara kwa mara.

“Nikiri vibaka eneo hili wanatusumbua sana, hasa wanafunzi, sisi tuna vikundi vya ulinzi na usalama, huwa tunaenda maeneo ambayo hayalindwi na eneo hili linalindwa kwa mujibu wa wenye chuo, ndiyo maana huwa hatulitembelei mara kwa mara,” amesema.