Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwanamke adakwa akituhumiwa kutupa mtoto chooni

Muktasari:

  • Diwani wa Kata ya Rau, Stallone Malinda amesema tukio hilo limewashtua wakazi wa eneo hilo na kuonyesha dalili za mmomonyoko wa maadili katika jamii.

Moshi. Mwanamke mmoja mkazi wa Mtaa wa Sabasaba, Kata ya Rau, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro anayefahamika kwa jina la Scholastica Ngowo (32), anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kutoa mimba na kutupa mtoto mchanga anayedaiwa kuwa na umri wa takribani miezi saba kwenye shimo la choo.

Taarifa za awali zinaeleza kuwa mwanamke huyo, ambaye ni mama wa watoto wanne, alikuwa mjamzito, lakini hajaonekana mtaani kwa siku kadhaa kabla ya kubainika kuwa alijifungua mtoto huyo kumtupa kwenye shimo la choo.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro, Jeremiah Mkomagi akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Juni 27, 2026, amesema mtoto huyo ameopolewa chooni akiwa ameshafariki dunia.

“Tulipopata taarifa tulifika eneo la tukio na kukuta mtoto mchanga ndani ya shimo la choo. Tulifanya jitihada za kuutoa mwili na baadaye kuukabidhi kwa taratibu nyingine za kisheria,” amesema Kamanda Mkomagi.

Akizungumzia tukio hilo, mama mzazi wa mtuhumiwa, Elizabeth Ngowo amesema amesikitishwa na tukio hilo akieleza kuwa halikutarajiwa na ni la kikatili.

Amesema hakuwa na taarifa za ujauzito huo wala tukio hilo, hadi alipofika eneo hilo na kuambiwa kilichotokea.

“Huyu aliyekamatwa ni mwanangu, nilikuwa sijui chochote. Nimekuja hapa nimeambiwa ametoa mimba. Kama angefanikiwa kujifungua, huyo angekuwa mtoto wake wa tano. Kwa nini afanye hivyo?” amesema.

Ameongeza kuwa mwanaye amekuwa akilea watoto wake wanne peke yake, jambo lililomuumiza sana kama mzazi.

“Amefanya tukio baya na la kikatili. Hawa watoto wanne amewalea peke yake, sasa sijui ni roho gani ya kikatili hii imemuingia,” amesema kwa uchungu.

Diwani wa Kata ya Rau, Stallone Malinda amesema tukio hilo limewashtua wakazi wa eneo hilo na kuonyesha dalili za mmomonyoko wa maadili katika jamii.

“Leo imekuwa ni majonzi makubwa kwetu wana Rau. Ni tukio lililotushtua sana na kuonyesha jinsi jamii inavyokosa hofu ya Mungu,” amesema.

Ameongeza kuwa tukio hilo ni la kikatili na linapaswa kuwa funzo kwa jamii, hususan wanawake wanaopata ujauzito, kutokufikia uamuzi wa mwisho unaohatarisha uhai wa mtoto.

“Mama zangu, dada zangu na wadogo zangu, hata kama unapitia changamoto gani, hustahili kutoa uhai wa kile ulichokibeba,” amesema.

Aidha, amesema suala hilo limeachiwa Jeshi la Polisi ili liendelee na uchunguzi na kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake.

Kwa upande wake, msimamizi wa Polisi Kata ya Rau, Asha Mbwambo amesema kitendo hicho ni cha kihalifu na hakikubaliki.

“Kutoa mimba ni kosa kisheria. Ikiwa mtu amekataa ujauzito, ni vyema kutoa taarifa kwenye vyombo husika badala ya kuchukua uamuzi wa kinyume cha sheria,” amesema.