Mwanamke apona ugonjwa wa ajabu

Betina Emmanuel mkazi wa Mtwara Manispaa akiwa nyumbani kwao baada ya matibabu ya vidole vilivyokuwa vikioza na kukatika vyenyewe. Picha na Florence Sanawa

Muktasari:

  • Mwanamke aliyekuwa akioza na kukatika vidole Manispaa ya Mtwara Mikindani amepatiwa matibabu yaliyosababisha miguu kuacha kuoza na kupona.

Mtwara. Mwanamke alieyugua ugonjwa wa ajabu wa kuoza na kukatika vidole vya miguuni kwako, amepona baada ya kupata matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Kwa mara ya kwanza, Mwananchi Digital ilifika nyumbani kwa mwanamke huyo Novemba 2021 na kumkuta akiwa ameifunika miguu yake kwa kitambaa na akishindwa kutembea, hata hivyo; ilipomtembelea jana, ilimkuta amepona tatizo hilo.

Awali Betina Emmanuel (30) ameiambia Mwananchi Digital kuwa amekatika vidole vya miguu baada ya kuugua ugonjwa wa ajabu huku ukimsababishia maumivu makali.

Alisema kuwa ugonjwa huo ambao umesababisha kukatika vidole saba vya mguu yake, ulianza kwa kubadilika rangi na kuwa nyeusi huku akipatwa na maumivu na makali.

“Kabla ya kidole kukatika, huwa napitia wakati mgumu sana; uanza kama kidonda na baadaye kidole kinakatika chenyewe, kwasasa mguu wangu wa kulia kimebaki kidole kimoja lakini mguu wa kushoto nnavyo viwili tu,” amesema.

Mwananchi ilikutana na mama wa mwanamke huyo Selesina Buru ambaye alisema kuwa mwanae amepona na anatembea mwenyewe baada ya kupata msaada kupitia vyombo vya habari na hivyo serikali kumuona na kufikshwa katika Muhimbili ambapo alipata matibabu.

“Hali ya mwanangu ilikuwa mbaya sana, zamani hata tiba hatukujua kama atapa lakini leo hii anatembea mwenyewe, hata sasa ukimuangalia; licha ya makovu aliyonayo, amebaki na vidole viwili tu miguuni,” amesema mama huyo na kuongeza; 

“Laiti tungejua tukaenda hospitali mapema, mtoto wetu asingeathirika sana kwakuwa wengi tulidhani kuwa ni ushirikina; tukapambana na waganga kumbe ni ugonjwa ambao unatiba. Sasa amepona na anatembea mwenyewe kwa miguu yake japo mguu mmoja umebakiwa na kidole kimoja,” amefafanua.

Mama huyo amewasihi watanzania kuwa makini kwa kusema: “Ni vema tukipata ugonjwa wowote twende hospitali ili tupate matibabu, tukianzia kwa waganga sio sawa yaani huyu kijana aliteswa na homa kali, miguu inaoza na vidole vinadondoka vyenyewe; kwakweli serikali imetusaidia sana, tulikuwa tunashindwa hata kula nae maana alikuwa anatoa harufu kali.”

Baada ya kuona kwenye vyombo vya habari, Wizara ya Afya, ikishirikiana na Serikali ya Mkoa wa Mtwara, walisaidina na kuhakikisha binti huyo anafika katika hospitlai ya Taifa ya Muhimbili na kupata matibabu yaliyomponya.