Ugonjwa wa ajabu wamkata vidole mwanamke Mtwara

Mkazi wa Mtwara, Betina Emmanuel (30) aliyekatika vidole saba vya miguu na kubakia na vidole vitatu akiwa nyumbani kwao. Picha na Florence Sanawa

Muktasari:

Mkazi wa Mtwara, Betina Emmanuel (30) amekatika vidole vya miguu baada ya kuugua ugonjwa wa ajabu huku ukimsababishia maumivu makali.

Mtwara. Mkazi wa Mtwara, Betina Emmanuel (30) amekatika vidole vya miguu baada ya kuugua ugonjwa wa ajabu huku ukimsababishia maumivu makali.

 Akizungumza na Mwananchi ilipotembelea nyumbani kwao Betina amesema kuwa ugonjwa huo umekuwa ukimsababishia maumivu makali.

Amesema kuwa ugonjwa huo ambao umesababisha kukatika vidole saba vya mguu, vilianza hubadilika rangi na kuwa vyeusi huku vikiwa na maumivu na makali.

“Kabla ya kukatika huwa napitia wakati mgumu sana na naumia yaani kinanza kidonda kinaenda mpaka kinakatika chenyewe kwasasa mguu wa kulia kimebaki kidole kimoja lakini mguu wa kushoto nnavyo viwili tu” amesema na kuongeza

“Nilipoenda hospitali nilipimwa ugonjwa wa ukoma na kisukari lakini majibu yalitoka kuwa sina ila pia niliambiwa ukiwa na ukoma kidole kikikatika huumii lakini huu ugonjwa unaumia kabisaa yaani silali”

Mama yake Betina, Modesta Daniel amesema kuwa mwanaye amekuwa akiteseka na ugonjwa huo mpaka ameshindwa kuhudumia watoto wake na ameshindwa kuishi na mzazi mwenzie.

“Hali hii imeanza muda mrefu tumefika hospitali tukaambiwa hana ugonjwa amepata matibabu mbalimbali hadi ikafikia kipindi akapona akaolewa na watoto wawili akapata tumefika ligula ndanda hospitali ambapo walisema sio ukoma na hawaoni ukoma ugonjwa huu unamtesa mwanangu” amesema

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Dk Joseph Kisala amesema kuwa mgonjwa huyo afikishwe kwenye kituo cha afya kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

“Aletwe sisi tutamchunguza na atapimwa tujue tatizo gani alilonalo kisha tutaangalia namna gani ya kumsaidia” alisema Dk Kisala