Mwanamke auawa, atupwa kichakani Njombe

Mwanamke auawa, atupwa kichakani Njombe

Muktasari:

  • Mwanamke mmoja ambaye hajatambuliwa haraka amekutwa na ameuawa na mwili wake kutupwa kichakani huku akiwa na majeraha maeneo ya shingoni na michubuko usoni.

Njombe. Mwanamke mmoja ambaye anakadiriwa kuwa na umri wa miaka 25 amekutwa ameuawa na mwili wake kushindwa kujulikana katika kijiji cha Muungano kilichopo kata ya Kifanya Halmashauri ya mji wa Njombe, mkoani Njombe.

Hayo yamesemwa leo Jumanne, Septemba 6, 2022 na Kamanda wa polisi mkoa wa Njombe, Hamisi Issah wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema jeshi hilo lilipata taarifa za mwili wa mtu kukutwa kwenye majani na walipofika eneo la tukio waliweza kuikuta maiti ya msichana huyo ikiwa na majeraha sehemu ya shingoni na michubuko usoni hali iliyowafanya jeshi hilo kuamini kuwa marehemu ameuawa.

"Baada ya kuukuta mwili wa marehemu na kuwatangazia wananchi mpaka muda huu hakutambulika. Ni jambo la ajabu kuona tukio la mauaji linatokea kwenye kijiji lakini marehemu anashindwa kutambulika na wenyeji wa eneo husika,” amesema.

Amesema mtuhumiwa mmoja anashikiliwa kwa kudhaniwa kuhusika na mauaji ya mwanamke huyo kutokana na mazingira yaliyopo hivyo ushahidi ukikamilika atafikishwa mahakamani.

Amewataka viongozi wa vijiji vyote mkoani Njombe kuhakikisha wanawatambua watu wa eneo lao ili kuepusha taharuki kama iliyojitokeza.

Amesema wananchi wa maeneo jirani na kijiji cha Muungano wafike katika hospitali ya halmashauri ya mjini Kibena ili kuutambua mwili wa marehemu.

Mwenyekiti wa kijiji cha muungano kilichopo kata ya Kifanya, Albeto Mkalawa amesema tukio hilo limetokea septemba 2 majira ya saa 12 asubuhi kwenye pori lililopo kitongoji cha Muungano.

"Tumeshirikisha makundi mbalimbali boda boda wakashindwa kumtambua, nikashirikisha wananchi wa kawaida wakashindwa kumtambua," alisema Mkalawa.

Aidha jeshi hilo limewaonya wamiliki wa mabasi ya kubeba wanafunzi ambao hawakupeleka magari yao kukaguliwa kufanya hivyo haraka iwezekanavyo vinginevyo watachukuliwa hatua.

"Ikifika saa kumi na mbili jioni wawe wameleta magari yao yaweze kukaguliwa kwani hatuwezi kushindana na sheria za nchi," amesema Issah.