Mwanamke mbaroni, adaiwa kumiliki SMG ya kienyeji

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Shadrack Masija, akionyesha bunduki aina ya SMG iliyokamatwa nyumbani kwa Shangwe Lodrick (35)

Muktasari:

  • Polisi mkoani Rukwa, inamshikilia mwanamke mmoja mkazi wa Mtaa wa Bangwe, Kata ya Izia, Tarafa ya Lwiche Manispaa ya Sumbawanga kwa tuhuma ya kukutwa akimiliki bunduki aina ya Shortgun.

Sumbawanga. Polisi mkoani Rukwa, inamshikilia Shangwe Lodrick (35), mkazi wa Mtaa wa Bangwe, Kata ya Izia, Tarafa ya Lwiche, Manispaa ya Sumbawanga, akidaiwa kumiliki bunduki aina ya Shotgun, iliyotengezwa kienyeji.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Shadrack Masija, amesema hayo leo Agosti 3, 2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, ambapo pia ametoa taarifa ya kukamatwa kwa pikipiki nne zilizoibwa na kutumika kwenye matukio ya uhalifu.

Kamanda Masija amesema bunduki hiyo iliyotengenezwa kienyeji ilikamatwa ikiwa pamoja na risasi 8 zinazotumika kwenye vitendo vya uhalifu.

"Wasamaria wema watupa taarifa ambapo polisi walifika nyumbani kwa mwanamke huyo na kufanya upekuzi na kukuta silaha hiyo ambayo inadaiwa imekuwa ikitumika kupora fedha kwenye visima vya mafuta na maduka yanayotoa huduma za kifedha kwa mitandao ya simu," amesema.

Amesema mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika ili sheria ziweze kuchukua mkondo wake.

Katika hatua nyingine, polisi imefanikiwa kukamata pikipiki sita ambazo ziliibwa maeneo tofauti tofauti mkoani hapa, pikipiki mbili kati ya hizo zimetambuliwa, huku watuhumiwa wakitarajiwa kufikishwa mahakamani.

Kamanda huyo amewataka wananchi walioibiwa pikipiki kufika kituo kikuu cha polisi Sumbawanga ili waweze kuzitambua pikipiki zao.

Mwisho.