Mwananchi lasifiwa kumuibua Mariam aliyekosa ada ya shule

  • Wa kulia ni Mwakilishi kampuni ya Mwananchi Habel Chidawali ambaye aliitwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka (kushoto) ili kupiga Picha ya pamoja na Mariam Mchiwa ambaye aliibuliwa na gazeti hili akitafuta fedha kwa ajili ya shule.

Muktasari:

  • Gazeti la Mwananchi lilimuibua Mariamu (19) aliyekuwa akisaka pesa kwa ajili ya kugharamia masomo yake ya kidato cha tano shule ya wasichana Songea kutokana na ufaulu wake wa daraja la kwanza kwa point 16.

Dodoma. Serikali mkoani Dodoma imeshukuru gazeti la Mwananchi kwa kuibua habari ya Mariamu Mchiwa ambaye anatakiwa kwenda masomoni Songea.

Mbali na Mkuu wa mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka, lakini Sheikh wa mkoa wa Dodoma Mustapha Rajabu amesema kama si gazeti la Mwananchi habari ya mtoto huyo isingeonekana mapema na kumsaidia kufikia lengo lake.

Gazeti la Mwananchi lilimuibua Mariamu (19) aliyekuwa akisaka pesa kwa ajili ya kugharamia masomo yake ya kidato cha tano shule ya wasichana Songea kutokana na ufaulu wake wa daraja la kwanza kwa point 16.

Viongozi hao walitoa kauli hiyo jana kwa nyakati tofauti baada ya baada ya kumkutanisha Mariamu na Wadau waliokubali kumsomesha kuanzia kidato cha tano hadi Chuo Kikuu.

Akizungumza leo Mei 26 katika halfa ya kukabidhi kwa watu waliojitolea kumsomesha ambao ni Chuo Kikuu cha Mwanza, Mkuu wa Mkoa Mtaka amesema habari za binti huyo zilimfanya aamue kubeba jukumu hilo yeye na viongozi wenzake mkoani kuhakikisha ndoto yake inatimia.

“Tuwashukuru watu wote ambao walifanikisha jambo hili, lakini wadau wetu wa Mwananchi pia karibuni hata tupige picha na binti huyu mmefanya kazi kubwa,” amesema Mtaka.

Mkuu wa mkoa amesema bado wapo wadau wengi wanaomiminika kumsaidia mtoto huyo ambapo jana alikabidhi Sh650,000 zilizoingizwa kwenye akaunti yake kwa ajili ya masomo.

Fedha hizo zilitoka kwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mwanza, Profesa Flora Fabiani ambao pia wanamsomesha lakini yeye alitoa kwa upande wake Sh200,000, Nyambura moremi Sh150,000 na benki ya Equit Sh300,000 na walimfungulia akaunti ambayo haina gharama za uendeshaji.

Mbali na wadau hao lakini mkuu wa mkoa alisema kuna watu wengi wanataka kumsaidia Mariam ambaye kwa sasa anaishi nyumbani kwa mbunge wa Kongwa Job Ndugai.

“Kwa sasa tunafanya mpango kuwafungulia bima ya matibabu wazazi wake baada ya kuona kweli wanahali ngumu, lakini mbunge wao na Spika Mstaafu Job Ndugai ameshazungumza nao na kuridhia binti akasome na binafsi yeye atabeba majukumu makubwa mtoto huyu kama mwanawe,” amesema Mtaka.

Makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Mwanza, Profesa Flora Fabian amesema licha ya uchanga wa chuo chao lakini jukumu la kuunga mkono wadau kwenye elimu ni lazo na wangetamani kufanya hivyo kwa sababu binti huyo amechaguliwa katika masomo ya sayansi ambayo wanapenda kudhamini.

Profesa Fabian amesema watakuwa na binti huyo katika gharama zote hadi watakapoona amefika Chuo kikuu na kumaliza masomo yake bila kukwama kwa jambo lolote.

Akizungumza mbele ya Mkuu wa mkoa, Mariam amesema ndoto yake ni kusoma na kufikia mafanikio ya kwenda kuisaidia familia yao yeye akitamani kuwa muuguzi.

Ametaja sababu za kutaka kazi hiyo kuwa ni kutokana na tatizo la kidonda alichonacho baba yake mzazi alichokipata tangu mwaka 1993 baada ya kufanyiwa upasuaji hivyo anaamini kuwa kuna mahali wataalamu walikosea.

“Mimi nataka kuwa muuguzi, na kweli ndoto hiyo ndiyo ninayo siku zote, sababu kubwa ni kitendo alichofanyiwa baba yangu na kwa kuzingatia mimi ndiyo niliyesoma kwetu basi nije niwasaidie familia na watu wengine,”alisema Mariamu.

Binti huyo alisema atasoma kwa bidii na maarifa kwani anataka kupata ufaulu wa daraja la kwanza kwa pointi 3 katika matokeo yake ya kidato cha sita.