Mwananchi yang’ara tuzo za Ejat, yazoa 12

Washindi wa tuzo za Ejat kutoka Mwananchi Communications Limited wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Bakari Machumu (aliyesimama katikati mwenye miwani) pamoja na viongozi wa wahariri wa Mwananchi

Muktasari:

  • Wakati waandishi wa mwananchi wakizoa tuzo 12 za Umahiri za Uandishi wa Habari (Ejat) zilizoandaliaa na Baraza la Habari Tanzania, wao wamesema ni chachu na motisha ya kufanya vyema zaidi.

Dar es Salaam. Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) imeshinda tuzo 12 usiku wa jana Jumamosi Julai 22, 2023 katika mashindano ya Tuzo za Umahiri za Uandishi wa Habari Tanzania (Ejat).

Katika kinyang'anyiro hicho kilichohusisha waandishi 92 nchini waliofika hatua ya mwisho, Mwananchi iliingiza waandishi 19 katika vipengele mbalimbali.

Tuzo hizo zimeandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa kushirikiana na wadau wengine.

Katika tuzo hizo, Pamela Chilongola amekuwa mshindi wa tuzo ya uchumi, biashara na fedha, Jumaa Issihaka ameshinda tuzo tatu ikiwemo ya habari za uchunguzi, kundi la wazi huku akichukua pia tuzo ya utawala bora na uwajibikaji kundi la mitandaoni.

George Helahela mshindi wa habari za takwimu upande wa mitandaoni, Janeth Joseph mshindi kipengele cha habari za haki za binadamu, , Kelvin Matandiko mshindi kipengele cha jinsia na watoto.

 Ephraim Bahemu ameshinda tuzo ya gesi, mafuta na madini, Mariam Mbwana Mshindi wa kipengele cha habari za walemavu, Baraka Loshilaaa na Herrieth Makweta washindi wa kipengele cha habari za Afya huku pia Baraka Loshilaa akishinda Kipengele cha uandishi wa habari za kodi, tozo na mapato.

Akizungumzia ushindi huo, George Helahela ambaye ameshinda kipengele cha uandishi wa takwimu mitandaoni amesema tuzo hizo zinatoa chachu kwa wanahabari kujikitika zaidi katika weledi wa taaluma.

"Kufanya hivi kunasaidia jamii inayotuzunguka kupitia kalamu zetu," amesema Helahela.

Kwa upande wake, Jumaa Issihaka amesema kuibuka mshindi wa tuzo tatu inamuongezea chachu na ari katika utendaji kazi wake.

"Ni kama motisha ya kufanya zaidi ya pale nilipofika, ukizingatia mimi ni mwandishi chipukizi na hii ni mara ya kwanza kushiriki tuzo hizi hivyo kilichopatikana ni kama kuonyesha kuwa naweza kufanya vyema zaidi ndani na nje ya nchi," amesema Issihaka.

Wengine walioingia fainali na kuibuka washindi wa pili na tatu ni Imani Makongoro, Josephine Christopher, Sadam Sadick, Elizabeth Edward, Hellen Nachilongo, Mussa Juma, Julius Mnganga, Tumaini Msowoya.