Mwandishi MCL azikwa Liwale

Mwakilishi wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Elias Msuya akiwa pembeni ya kaburi la aliyekuwa mwandishi wa gazeti la Mwananchi mkoani Lindi, Mwanja Ibadi pamoja na ndugu wa marehemu wilayani Liwale mkoani humo.

Muktasari:

  • Mwandishi wa kujitegemea, Mwanja Ibadi aliyefariki Mei 27 amezikwa jana Jumapili kijijini kwao Kiangara wilayani Liwale Mkoa wa Lindi.

Liwale. Mwandishi wa gazeti la Mwananchi, Mwanja Ibadi aliyefariki Mei 27 amezikwa jana Jumapili kijijini kwao Kiangara wilayani Liwale Mkoa wa Lindi.

Mazishi hayo yamehudhuriwa na waandishi wa habari, viongozi wa Manispaa ya Lindi na wanakijiji.

Akizungumzia mazishi hayo leo Mei 29, 2023 kaka wa marehemu, Sikudhani Mbega ameishukuru Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd kwa ushirikiano na familia yao katika msiba huo.

"Japo hamkuwahi mazishi, tunawashukru kwa kufika kutufariji, huu ndio undugu," alisema Mbega akimweleza mwakilishi wa MCL aliyefika kijijini hapo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Lindi Regional Press Club, Ahmad Mmow alishukuru MCL ushirikiano.

"Poleni sana kwa msiba, mmepata pigo. Ibadi alionekana vizuri kitaaluma kutokana na utaratibu wa Mwananchi wa kufanya kazi hasa katika utafutaji wa habari na hiyo inaifanya Mwananchi iwe mbele," alisema.

Awali, akizungumza katika msiba huo juzi Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa habari mkoani Lindi, Fatuma Maumba alisema wiki iliyopita Mwanja alilazwa katika hospitali ya Ngudu.

Alisema baadaye alihamishiwa Hospitali ya Nyangao na kuruhusiwa baada ya siku kadhaa, kabla ya hali yake kubadilika tena.

Baada ya hali hiyo, Fatuma alisema Mwanja alipelekwa tena katika Hospitali ya Nyangao na ndiko alikofariki.