Mwanzo, mwisho uamuzi wa Jaji Siyani

Mwanzo, mwisho uamuzi wa Jaji Siyani

Muktasari:

  • Wakati Kamishna Msaidizi wa Polisi, Ramadhani Kingai akitoa ushahidi wa jinsi mshtakiwa wa pili, Adam Kasekwa alivyokamatwa Moshi, mkoani Kilimanjaro, Agosti 5, 2020, mabishano makali ya kisheria yalizuka baada ya mawakili wa utetezi kupinga maelezo ya mshtakiwa huyo yasipokelewe mahakamani kama kielelezo.

Dar es Salam. Katika gazeti lako la Mwananchi leo tunakuletea mapitio ya uamuzi wa kesi ndogo iliyoibuka ndani ya kesi ya msingi ambamo mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu waliokuwa askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wanashtakiwa kwa makosa uhujumu uchumi na kupanga kufanya ugaidi. Endelea…

Wakati Kamishna Msaidizi wa Polisi, Ramadhani Kingai akitoa ushahidi wa jinsi mshtakiwa wa pili, Adam Kasekwa alivyokamatwa Moshi, mkoani Kilimanjaro, Agosti 5, 2020, mabishano makali ya kisheria yalizuka baada ya mawakili wa utetezi kupinga maelezo ya mshtakiwa huyo yasipokelewe mahakamani kama kielelezo.

Kingai alikuwa akieleza jinsi jitihada za kumtafuta mshukiwa mwingine aliyejulikana kwa jina la Moses Lijenje, kwa usaidizi wa Kasekwa zilivyoshindwa.

Alisema katika ushahidi wake kuwa baada ya kushindwa kumpata Lijenje, Kasekwa anayejulikana pia kwa jina la Adamoo, alisafirishwa hadi katika Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam ambapo alihojiwa na kudaiwa kukiri kula njama za kupanga kutenda vitendo vya kigaidi.

Baada ya ushahidi huo, Kingai aliitaka mahakama ipokee maelezo ya onyo ya Kasekwa aliyoyatoa Agosti 7, 2020, kama sehemu ya ushahidi wake.

Hapa ndipo timu ya mawakili wa utetezi wakasimama kupinga kupokelewa kwa maelezo hayo wakitoa sababu mbili.

Katika hoja ya kwanza, walidai kuwa maelezo hayo nje ya muda unaoruhusiwa kinyume na vifungu cha 50 (1) (a), (b) 51 na 52 vya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Kifungu cha 51 (1) (a) kinataka maelezo ya mtuhumiwa wa makosa ya jinai yachukuliwa ndani ya muda wa saa nne baada ya kutiwa nguvuni.

Hata hivyo, kifungu kidogo cha (a) kimeweka wazi kuwa endapo mtu anashikiliwa na muda wa saa nne lakini akawa hajashtakiwa kwa kosa analoshikiliwa nalo, kiongozi wa upelelezi anaweza kuongeza muda wa mahojiano kwa saa zisizozidi nane.

Kwa mujibu wa kifungu kidogo cha (b), ofisa wa upelelezi anaweza pia kupeleka maombi kwa hakimu kuongeza muda zaidi isipokuwa afanye hivyo kabla muda ulioongezwa haujaisha.

Pili, mawakili wa utetezi walitaka maelezo yake yasipokelewe wakidai mteja wao aliteswa kabla na wakati akichukuliwa maelezo.

Kwa kuzingatia uhalisia wa mapingamizi hayo, mawakili wa Jamhuri na wale wa utetezi walikubaliana kuwa kulikuwa na haja ya kuletwa ushahidi mahakamani ili kujua ukweli wa mapingamzi hayo.

Katika hatua hiyo, Jaji aliyekuwa akisikiliza kesi Mustapha Siyani aliamua kuisimamisha kesi ya msingi na kuamuru kufanyika kwa kesi ndani ya kesi.

Wakati wa usikilizwaji wa kesi ndani ya kesi, kila upande uliandaa mashahidi watatu kuthibitisha madai yao.


Ushahidi wa Jamhuri

Ushahidi wa Jamhuri ni kwamba baada ya kukamatwa Agosti 5, 2020, Kasekwa hakuweza kuhojiwa ndani ya saa nne zinazotakiwa na sheria kwa madai kuwa upelelezi ulikuwa bado ukiendelea.

Ushahidi wa Kingai na Inspekta Mahita Omary ulionyesha kuwa baada ya ‘kutonywa’ na msiri kuhusu uwepo wa Kasekwa na wenzake wawili katika eneo la Rau Madukani, Moshi Mjini, kipaumbele chao cha kwanza kilikuwa ni kuwakamata watuhumiwa wote watatu.

Hata hivyo, alidai baada ya kufika walipokuwepo walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili tu akiwemo Kasekwa. Alidai mtuhumiwa wa tatu aliyejulikana kwa jina la Moses Lijenje alitoweka na hakuweza kupatikana.

Kwa mujibu wa Kingai na Mahita, Kasekwa aliridhia kujitolea kuwaongoza polisi katika kumtafuta Lijenje. Kazi ya kumsaka Lijenje iliwapeleka hadi eneo la Bomang’ombe, KCMC, Majengo and hoteli ya Aishi iliyopo Kata ya Machame bila mafanikio.

Mashahidi hao walieleza kuwa baada ya kufika saa 4:30 usiku walirudi Kituo Kikuu cha Polisi, Moshi ambamo Kasekwa alihifadhiwa.

Ushahidi wao unaonesha kuwa kazi ya kumsaka Lijenje iliendelea tena siku iliyofuata (Agosti 6, 2020) kwa msaada wa Kasekwa. Siku hiyo, timu ya wapelelezi ilikwenda katika sehemu tofauti ikiwemo Kituo Kikuu cha Mabasi, Moshi na eneo la Sakina, Arusha ambapo dada yake Lijenje alidaiwa kuishi.

Ilipofika saa 2 usiku bila dalili yoyote ya kumpata Lijenje, amri ilidaiwa kutolewa na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwamba watuhumiwa waliokamatwa wasafirishwe hadi Dar es Salaam ambapo kesi yao iliripotiwa kwanza na faili ya uchunguzi lifunguliwe.

Wote, Kingai na Mahita walidai kuwa walianza safari na kufika Dar es Salaam Agosti 7, 2020 saa 11:30 alfajiri ambako Kasekwa alikabidhiwa kwa mpelelezi aliyetajwa kwa jina la Msemwa na kuhifadhiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam.

Ushahidi wa Kingai unaonyesha kuwa wakiwa Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, na baada ya kujulishwa haki zake za kisheria, Kasekwa alihojiwa kuanzia saa 1:30 asubuhi hadi saa 3 asubuhi siku hiyo hiyo walipowasili kutokea Moshi.


Hoja za utetezi

Katika utetezi wake licha ya kukiri kuwa alikuwa na Lijenje eneo la Rau Madukani alipokamatiwa, Kasekwa alikataa ushahidi kuwa aliiongoza timu ya polisi katika maeneo mbali mbali ya Moshi na Arusha katika kumsaka Lijenje.

Pili, alikataa kuwa alipelekwa moja kwa moja Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam wakitokea Moshi. Kwa mujibu wa Kasekwa, alianza kupelekwa Kituo cha Polisi, Tazara.

Soma toleo la kesho kujua zaidi

hoja za upande wa mashtaka

Adai kuteswa

Kasekwa alidai kuwa baada ya kukamatwa maofisa wa polisi walimtesa vikali na wakati akiteswa walilazimishwa kutoa baadhi ya maelezo. Alidai yote hayo yalitendeka akiwa Moshi.

Maelezo mengine ya utetezi kuhusu kilichompata Kasekwa baada ya kufikishwa Dar es Salaam ni kwamba alishikiliwa katika Kituo cha Polisi Tazara kabla ya kupelekwa Kituo cha Polisi, Mbweni ambako alidai kutishiwa kusaini baadhi ya nyaraka Agosti 9, 2020.

Maelezo kuwa Kasekwa aliteswa yaliungwa mkono na ushahidi wa mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo Mohamed Ling’wenya na Lilian Kibona ambaye ni mke wa Kasekwa.

Wakati Ling’wenya alidai alimsikia Kasekwa akilia kwa uchungu kwa kile alichokielezea kuwa kwa “sauti ya zege” wakati akiwa Kituo cha Polisi, Moshi, Kibona alidai kuwa alimwona Kasekwa akiwa na makovu katika mikono yote siku alipomtembelea katika mahabusu ya gereza la Segerea.

Mbali na makovu, Kibona alidai pia Kasekwa alionekana kutokuwa na afya na alitembea kwa kuchechemea.


Hoja za Jamhuri

Kuhusu hoja kuwa maelezo ya Kusekwa yalichukuliwa nje ya muda, Wakili wa Serikali Mwandamizi Robert Kidando alisema maelezo ya Kasekwa yalichukuliwa ndani ya muda wa kisheria kwa kuwa kifungu cha 50 (2) hakihesabu muda uliotumiwa na wapelelezi kumpeleka mtuhumiwa kituoni au sehemu nyingine kwa masuala ya upelelezi.

Hivyo aliitaka mahakama isihesabu muda uliotumiwa na wapelelezi katika kuamua pingamizi hilo.

Kuhusu hoja ya kwa nini Kasekwa alihojiwa Dar es Salaam badala ya Moshi alipokamatiwa, upande wa Jamhuri ulidai kuwa hiyo ilifanyika kwa sababu ya unyeti wa kosa alilotuhumiwa na ugumu wa upelelezi ikizingatiwa kosa lilidaiwa kufanyika mikoa tofatuti.

Kuhusu madai kuwa Kasekwa aliteswa, Kidando alidai kuwa upande wa utetezi haukuwa na mashaka ya msingi kuhusu uhiari wa mshitakiwa huyo kutoa maelezo.

Alidai ushahidi wa Kasekwa ulikwepa pingamizi hilo, alishindwa kumhoji shahidi wa Jamhuri katika mambo ya msingi. Wakili huyo alihoji pia kuaminika wa ushahidi wa utetezi katika hoja hiyo.

Soma toleo la kesho kujua zaidi hoja za upande wa mashtaka katika kujibu mapingamizi ya utetezi.