Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwarobaini Soko la Mabibo wapatikana

Muktasari:

  • Hali ya kukodi mabuti kuingia soko la Mabibo inaenda kuisha, baada ya Manispaa ya Ubungo, kumpata mkandarasi wa kujenga barabara ya kuingia na kutokea sokoni humo kwa kiwango cha zege.

Dar es Salaam. Ile hali ya kukodi mabuti kuingia Soko la Mabibo, sasa inaenda kuisha, baada ya Manispaa ya Ubungo, kumpata mkandarasi wa kujenga barabara ya kuingia na kutoka sokoni hapo kwa kiwango cha zege.

Sambamba na hilo, pia mkandarasi huyo atajenga mitaro ambayo itakuwa ikiruhusu maji yaliyokuwa yakituwama ndani kutoka nje kwa urahisi.

Hayo yamesemwa leo Jumamosi, Septemba 7, 2023 na Meneja wa soko hilo, Samson Lugala, katika mahojiano maalum na Mwananchi Digital, iliyofika sokoni hapo, ambapo ilitaka kujua kinachoendelea tangu soko hilo lirudishwe chini ya usimamizi wa Manispaa hiyo.

Lugala amesema katika ukarabati huo, Manispaa imetanga Sh600 milioni, ambapo mbali na ujenzi wa barabara na mitaro, pia itajenga choo cha kisasa na mashedi kwa ajili ya kukaa wafanyabiashara.

 “Mkandarasi ameshapatikana na tayari tumeshamuonyesha eneo la kufanyia kazi, nadhani kuanzia wiki ijayo ataanza na tumempa muda wa mwezi mmoja awe amemaliza,” amesema Lugala.

Tangu mwaka 2020 soko hilo lilikuwa likiendeshwa na wafanyabiashara wenyewe kabla ya Agosti, 2023 ambapo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, aliamua kulirudisha mikononi mwa Manispaa ya Ubungo.

Wafanyabiashara hao walikuwa wakiliendesha baada ya kukabidhiwa na Hayati John Magufuli, alipokuwa kwenye mkutano wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 katika viwanja vya Barafu Mburahati, mkoani Dar es Salaam

Hatua ya Chalamila kulirudisha soko hilo, ni kuwepo kwa tuhuma kuwa viongozi wa wafanyabiashara waliopewa dhamana ya kulisimamia soko hilo wamekuwa kikwazo katika utoaji wa huduma bora huku wakituhumiwa kufanya vitendo vya ubadhirifu wa fedha.

Uwepo tope sokoni hapo, haukuwa tu kero kwa wafanyabiashara bali hata kwa wateja waliokuwa wakienda kupata mahitaji sokoni yao.

Awali wateja hao walilazimika kukodisha mabuti kutoka kwa watu waliokuwa wamejipanga nje ya soko hilo, ambapo walitakiwa kulipa kati ya Sh1000 ikiwa watakodi kwa muda, huku wale wa siku nzima wakilipishwa Sh7000.

Na kwa yule anayetakiwa kuoshwa miguu baada ya kukutana na dhahma ya tope sokoni hapo, alitakiwa huku kwa anayevaa kwa siku nzima, alitakiwa kulipa Sh200.

Athuman Kileo, alisema wanayaona mabadiliko ya kasi ndani ya mwezi mmoja na kueleza hayo ndio maendeleo waliokuwa wanayatamani siku zote kuyaona sokoni hapo.

Pia aliyewahi kuwa mwekahazina wa soko hilo, Edwin Lymo, alisema wanaridhika na juhudi ambazo Manispaa inazifanya katika kuliboresha soko hilo na kuahidi kuendelea kuwapa ushirikiano kila watakapohitajika.

Kwa upande wa wateja wanaoenda kupata manunuzi hapo akiwemo Eva Enock, alipongeza hatua ya ukarabati huo, na kueleza itawapunguzia adha ya kwenda kupata bidhaa zinazopatikana kwa wingi sokoni hapo ukilinganisha na masoko mengine ikiwemo.

“Ukiacha manunuzi ya vitu, pia kupunguza gharama za kukodi mabuti ambayo pia yalikuwa yakihataraisha usalama wa afya zetu,” amesema Eva.