Mwasu, dereva wa bajaj mwenye shahada mbili

Mwasu, dereva wa bajaj mwenye shahada mbili

Muktasari:

Tofauti na mawazo ya wengi kuwa ukisoma hadi chuo kikuu lazima uajiriwe, Mwasu Mavere ameonyesha upande mwingine wa shilingi, kwamba unaweza kujiajiri na kufanikiwa zaidi.

Dodoma. Tofauti na mawazo ya wengi kuwa ukisoma hadi chuo kikuu lazima uajiriwe, Mwasu Mavere ameonyesha upande mwingine wa shilingi, kwamba unaweza kujiajiri na kufanikiwa zaidi.

Licha ya kuwa na shahada ya uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), yeye ameamua kuwa dereva wa pikipiki ya miguu mitatu (bajaji) akisafirisha abiria katikati ya makao makuu ya nchi, Dodoma.

Mwasu anasema wasomi wengi wanatembea na bahasha miaka hadi mitatu bila kupata kazi, kumbe wangeuza hata karanga zingewaingizia kipato badala ya kuzunguka na vyeti.

Hata hivyo, anasema mfanyabiashara msomi ni tofauti na asiyesoma, kwa kuwa ile elimu aliyonayo msomi anaitumia kufanya vizuri kwenye biashara zake.

“Kuna wasomi wengi wanaendesha bajaji na bodaboda na wapo wengine wengi mtaani wanatafuta kazi, hawajajua kuwa kuna kazi ya kuendesha bajaji na kujipatia fedha kama walioajiriwa, hivyo niwatake waache kuchagua kazi,” alisema Mwasu alipozungumza na Mwananchi.

Mwasu alianza shughuli za usafirishaji abiria Desemba 2018 katika eneo la eneo la Royal Village, Dodoma lakini baada ya muda alihamia katikati ya mji ili kupata abiria wa pande zote.

“Elimu yangu ni masters, lakini mshahara mdogo niliokuwa nalipwa ndio uliosababisha nikaamua kuacha kazi na kujishughulisha na biashara mbalimbali ikiwemo kuuza nguo na hatimaye nikaanza kuendesha bajaji,” anasema.

Mwasu, mama wa watoto wawili anasema mshahara aliokuwa analipwa ambao haukukidhi mahitaji yake wala kuendana na kiwango chake cha elimu, ulisababisha akaichukia ajira akaamua kujiajiri mwenyewe.

Alisema mwaka 2009 alihitimu shahada ya sociology and political science nchini Kenya na baada ya hapo alirudi nchini na kufanya kazi katika NGOs mbalimbali.

Ilifopika mwaka 2011 aliamua kujiendeleza katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) huku akiendelea kufanya kazi. Alihitimu mwaka 2013 shahada ya uzamili katika utawa (Masters of public adminstration).

Alisema wakati anafanya kazi kwenye shirika lisilo la kiserikali la Afnet alikuwa programme officer na field officer baada ya muda akahamia katika shirika jingine la Ngonedo ambapo alikuwa monitoring and evaluation officer (ufuatiliaji na tathmini).

Mwasu alisema katika kipindi alichofanya kazi hakuwa na mshahara uliokuwa unazidi Sh390,000 kwa mwezi, ambao amesema haukuwa unakidhi mahitaji yake.

Alisema kipindi hicho anafanya kazi alikuwa na mtoto mdogo, hivyo kutokana na mahitaji yake kuwa mengi na mshahara mdogo alipomaliza shahada ya uzamili aliamua kuacha kazi na kuanzisha biashara mbalimbali ikiwemo kuuza nguo.

“Hela hiyo haikuwa inakidhi mahitaji yangu, mwisho wa siku nikaona ili nisiingie kwenye vishawishi vya kuiba fedha ofisini ili kukidhi mahitaji, bora niache kazi, niliona ni bora kujiajiri mwenyewe kuliko kuajiriwa kwani nilichokuwa ninalipwa hakilingani na elimu yangu.

“Wakati huo nafanya kazi, nilikuwa nakusanya hela kidogo kidogo na kuna siku nilienda field, pesa niliyolipwa na zile akiba zangu nikaamua kuanzisha biashara kwa mtaji wa Sh400,000. Nilikwenda Kariakoo (Dar es Salaam na kuchukua mzigo wa nguo na kuja kuuza Dodoma,” alisema Mwasu.

Alisema biashara yake ilikuwa vizuri na alikuwa anaingiza fedha kuliko zile alizokuwa analipwa wakati ameajiriwa.

Biashara hiyo aliifanya kwa muda mrefu hadi akawa anasafiri kwenda China pamoja na wafanyabiashara wengine kuchukua mzingo wa nguo na kuuza nchini.

“Katika biashara kuna kuinuka, lakini pia unaweza kushuka. Biashara yangu ilikuja kuwa mbovu nikawa napata hasara, si kila siku ni kupata faida, hasara kwa mfanyabiashara haikwepeki nawakati huo tayari nilikuwa nishapata mtoto wa pili.

“Licha ya hasara hiyo, sikukata tamaa badala yake nikaamua kubadilisha kazi ya kufanya. Niliamua kuachana na biashara kabisa na kuwa dereva bajaj,” alisema.


Kilichomfanya aendeshe bajaji

Mwasu aliamua kuwa dereva bajaji kwa kuangalia fursa baada ya kuona wengine wanaofanya biashara hiyo wanafanikiwa, akitolea mfano rafiki yake aliyekuwa anaendesha bajaj ambaye alimhamasisha kufanya kazi hiyo.

“Nikiwa dereva bajaj najua kuwa ni lazima mtu asafiri, tofauti na kuvaa nguo. Mtu anaweza kununua nguo baada ya muda mrefu,” alisema.

Alisema alipata taarifa kuwa Benki ya CRDB inakopesha bajaj kwa Sh6 milioni, na katika kufuatilia alitakiwa kuwa na mdhamini ambaye ni mwajiriwa na mshahara wake unapitia katika akaunti ya taasisi hiyo, ili akishindwa kurejesha wawe wanamkata fedha hiyo.

Mwasu alisema baada ya kukamilisha vigezo hivyo, alikabidhiwa bajaji na kuanza kufanyia biashara tangu Desemba 2018.

Alisema ‘kijiwe’ chake cha kwanza kilikuwa katika eneo la hoteli ya Royal Village, lakini baada ya muda akaamua kuhamia maeneo ya mjini ili kupata abiria zaidi.

Desemba 2019 alimaliza marejesho kwa muda uliokuwa umepangwa na kuanzia hapo akawa mmiliki halali bajaj hiyo.


Manufaa ya bajaji

Amasema usafiri huo umemsaidia kwa kiasi kikubwa kupanga mipango yake kupitia fedha anazozipata -- analisha familia yake na anasomesha watoto shule binafsi.

Mwasu aliyesema kwa sasa hana mawasiliano na baba watoto wake, mtoto wake wa kwanza yupo darasa la pili na mwingine yupo chekechea na anatarajia kujenga nyumba yake ya kuishi kwa fedha anazozipata kwenye usafiri huo.

Mwasu anasema mipango yake kwa siku ni kupata Sh50,000, lakini kuna siku anapata zaidi ya hizo na wakati mwingine anaishia kupata hata Sh20,000.


Changamoto aipatayo

Mwasu anazungumzia kile anachoita unyanyasaji unaofanywa na trafiki barabarani kuwakamata na kuwasingizia makosa mbalimbali ikiwemo kuzidisha abiria.

Mwasu anasema aliwahi kukamatwa na kusingiziwa kuwa alibeba abiria saba kwenye bajaji yake, kitu ambacho alisema haikuwa kweli, kesi hiyo ilifika hadi mahakamani lakini alionekana hakuwa na kosa lolote.

“Upo uonevu unaofanywa na trafiki hata kama huna kosa wanakusingizia makosa, ingekuwa ni mtu wa kukata tamaa baada ya kufikishwa mahakamani asingeendelea na kazi hiyo, ila mimi ni strong woman (mwanamke jasiri) ndio maana bado napambana,” alisema na kuongeza.

“Tumekuwa tukipakia abiria kwa Sh500 ukitumia mfumo huo unapata pesa nyingi kuliko ukiwa unasubiri wanaokukodi.