Mwelekeo hali ya hewa kwa siku 10 zijazo nchini

Muktasari:
- Kulingana na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa utabiri wa saa 24 zijazo imetoa angalizo la mawimbi makubwa yanayofikia mita mbili kwa baadhi ya maeneo ya ukanda wa Pwani ya kaskazini mwa bahari ya Hindi yenye mikoa ya Tanga, Dar es Salaam na Pwani ikijumuisha visiwa vya Mafia, Unguja na Pemba.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetaja kanda nane nchini zitakazopitia hali ya ukavu na vipindi vya mvua kwa kipindi cha siku 10 kuanzia leo Julai mosi, 2025.
TMA kupitia taarifa yake imeeleza, kanda ya Ziwa Victoria yenye mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Mwanza, Simiyu na Mara itakuwa na hali ya ukavu.
“Nyanda za juu kaskazini-mashariki yenye mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro nayo itakuwa na hali ya ukavu kwa ujumla,” imeeleza taarifa hiyo.
Pia mikoa ya Pwani ya kaskazini inayojumuisha Tanga, maeneo ya kaskazini mwa Morogoro, Pwani na Dar es Salaam, visiwa vya Unguja na Pemba kunatarajiwa uwepo wa vipindi vya mvua nyepesi na upepo mkali kwa maeneo machache.
Vilevile, Magharibi mwa Tanzania yenye mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora pia matarajio ni hali ya ukavu.
“Kanda ya kati yenye mikoa ya Dodoma na Singida matarajio ni hali ya ukavu, Nyanda za juu Kusini-magharibi, mikoa ya Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa kunatarajiwa hali ya ukavu,” imeeleza taarifa ya TMA.
Kwa upande wa Pwani ya kusini yenye mikoa ya Mtwara na Lindi matarajio ni hali ya ukavu kwa ujumla na vipindi vya upepo mkali vinatarajiwa.
Katika maeneo ya kanda ya kusini yenye mikoa ya Ruvuma na Maeneo ya kusini mwa Morogoro, TMA imeonyesha matarajio ya hali ya ukavu.