Mikoa hii ijipange kwa baridi Juni hadi Agosti

Muktasari:
- Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetangaza baridi kali Juni hadi Agosti katika mikoa sita, wananchi watakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya baridi.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema kuanzia Juni hadi Agosti, 2025 kutakuwa na baridi kali na ya wastani katika mikoa sita nchini.
Pia, maeneo mbalimbali nchini yatashuhudia joto, mvua zisizotabirika na kipupwe, huku athari ikitajwa kuwa ni magonjwa yanayohusiana na hali ya hewa ya baridi kama vile homa ya mapafu na magonjwa ya mifugo.
Taarifa hiyo imetolewa na TMA kupitia tovuti yake, ikiwa ni uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa hali ya joto, upepo na mvua msimu wa Juni hadi Agosti 2025.
“Hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi. Hata hivyo, hali ya baridi ya wastani hadi baridi kali inatarajiwa katika maeneo ya mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Singida na maeneo ya magharibi mwa Mkoa wa Dodoma,” imeeleza taarifa hiyo.
Taarifa ya TMA imesema vipindi vya baridi zaidi vinatarajiwa kujitokeza Julai na vipindi vya mvua za nje ya msimu vinatarajiwa katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria, ukanda wa mwambao wa Pwani na visiwa vya Unguja na Pemba.
Kuhusu kipupwe, TMA imesema miezi hiyo itatawaliwa na upepo wa wastani utakaovuma kutoka kusini mashariki mwa maeneo mengi ya nchi na vipindi vichache vya upepo mkali.
Upepo utakuwa unavuma kutoka kusini (upepo wa kusi) hususani katika kipindi cha Juni na Julai, 2025 kwa maeneo ya ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi na maeneo ya nchi kavu.
“Magonjwa yanayohusiana na hali ya hewa ya baridi kama vile homa ya mapafu na magonjwa ya mifugo yanaweza kujitokeza, ingawa kwa kiasi kidogo, hali ya vumbi linalosababishwa na upepo katika baadhi ya maeneo litasababisha uwepo wa magonjwa ya macho,” imeeleza taarifa ya TMA.
Ushauri wa kitaalamu
Akizungumza na Mwananchi, daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa upumuaji, Elisha Osati amesema baridi inapokuwa kali kuna uwezekano wa kuleta mabadiliko kwenye njia ya hewa na mapafu, hivyo kurahisisha wadudu kusafiri.
Amesema hali hiyo inapotokea inasababisha kifua, mafua, homa na hata homa ya mapafu ambayo huwasumbua zaidi watoto kutokana na kushindwa kuhimili mabadiliko hayo.
"Ni kipindi ambacho watu wanapaswa kuwa makini na kuongeza uangalizi kwa watoto, hasa wadogo kabisa wahakikishe muda wote wamevaa nguo ambazo zinakinga miili yao dhidi ya baridi na ambazo zitasaidia pia kuhifadhi joto,” amesema.
Amesema ngozi ni vyema ikapakwa mafuta ya mgando ili kuikinga na baridi.
“Hili linapaswa kuzingatiwa hata na watu wazima kwa sababu baridi haichagui iingie kwa nani na wakati gani," amesema.
Dk Osati amesema kutokana na hali hiyo ya hewa inashauriwa kuviepuka vyakula vya baridi na vilivyopoa baada ya kupikwa muda mrefu.
"Kipindi hiki vyakula viliwe vikiwa vya moto, vikipoa kuna uwezekano wa wadudu kuingia na vikiwa na mafuta vikipoa yale mafuta yataganda, hivyo havitakuwa sahihi katika wakati huu wenye baridi,” amesema.
Amesema kundi lingine linalopaswa kujihadhari zaidi katika kipindi hiki ni wenye matatizo ya pumu, kifua, magonjwa ya moyo na mengine yanayohusisha mfumo wa upumuaji.
Dk Osati amesema: "Ikitokea mtoto amebanwa na kifua huna sababu ya kusubiri, mpeleke kwenye kituo cha afya kwa ajili ya uangalizi wa wataalamu."