Mwendokasi pasua kichwa, abiria wasota vituoni


Muktasari:

  • Tofauti na matarajio ya wengi ya kupata usafiri wa haraka, usafiri huo sasa umegeuka kuwa kero, kwani abiria wamekuwa wakisota vituoni kwa muda mrefu bila kuyaona mabasi.

Dar es Salaam. Kusubiri mabasi kwa muda mrefu vituoni ni moja ya adha wanazokumbana nayo abiria wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) jijini hapa huku wakistaajabu kuona mabasi mengine yakipita bila abiria.

Kwa mujibu wa abiria, vituo vyenye changamoto ni, Baruti, Stop over, Manzese, Tiptop, DIT, Kibaha, Mapipa, Kibamba shule na kwa komba.

Kaimu Meneja wa Mipango ya Usafirishaji Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (DART) Mohammed Kuganda alikiri uwepo wa malalamiko ya msongamano wa abiri vituoni sababu kubwa ni uhitaji wa usafiri huo kuongezeka.

Hali hiyo imejidhihirisha leo Oktoba 11 katika kituo cha mabasi yaendayo haraka kituo cha Kimara, ambapo Mwananchi ilishuhudia idadi kubwa ya abiria wakisubiri usafiri bila mafanikio.

Wengi wa abiria wliokuwepo eneo hilo majira ya saa tatu walikuwa wale wanaotoka Kibaha kufika hapo kwa ajili ya kiinganisha gari za kwenda Karikoo, Kivukoni na maeneo mengine ya jiji.

Zuhura Meck aliyetokea Kibaha alisema wanateseka kutokana na uwepo wa magari machache huku abairua wakiwa wengu.

"Hali hii ya kuteseka sio asubuhi tuhata jioni wakati wa kurudi nyumbani witi wangu waongeze magari,sio mtu unalipa halafu unaingia kituoni unakaa mida mrefu bila kupata gari," alisema Zuhura

Baadhi ya abiria waliozungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti walisema wanalazimika kuondoka kwenye vituo na kupanda usafiri mwingine wa daladala, bajaji au bodaboda baada ya kusubiri usafiri kwa wastani wa saa mbili.

“Nilikuwa natoka Kibaha niunganishe mabasi hadi Ubungo kero niliyoipata ni kukaa muda mrefu, kuanzia saa nne mpaka saa sita na nusu nasubiri basi, nilishindwa kutafuta njia nyingine kwasababu nilikwisha kulipa fedha,” alisema Mwajuma Hamis mkazi wa Kibaha.

Naye Haron James mkazi wa Kimara alisema majira ya asubuhi na jioni kero kubwa ni mabasi kujaza kwa kiasi kikubwa na kuanzia saa nne na hadi jioni adha inayofuata ni mabasi kuchelewa kuchukua abiria vituoni na mengine  kupita bila abiria.

“Unakaa kituoni ukisubiri kwa zaidi ya saa mbili alafu unaliona basi tupu linakupita na linakwenda kugeuza linakupita tena, hiyo ni kero kubwa, kwanini hayo mabasi yasitupeleke kuwahi tunapokwenda sisi kama wana mambo yao wanayafanye baada ya kutusaidia sisi,”alisema.

Kwa upande wake, Ramadhan Juma mkazi wa Magomeni alisema kusubiri muda mrefu mabasi ni changamoto ya muda mrefu.

 “Japo huu usafiri una msaada mkubwa lakini dosari zilipo zuitafutiwe ufumbuzi kuwepo na watoa huduma ambao wanaratibu mabasi kufika kituoni, huu utaratibu wa mabasi kutupita wakati tumejazana kituoni sio sawa,”alisema.

Wakati hali ikiwa hivyo, mjini Kibaha, changamoto kubwa ni uchache wa mabasi, foleni na wakati mwingine mtandao kusumbua na abiria kushindwa kukata tiketi.

"Nilifika kituoni saa mbili asubuhi, nikakuta hakuna huduma ya kukata tiketi, niliambiwa nitoke Kibaha Stendi hadi kituo cha Njuweni kwa ajili ya kukata tiketi," alisema Gaspar Robert.

Tatizo la mtandao nalo linatajwa na Rukia Mosses mkazi wa Kibaha ambaye alisema wakati mwingine abiria wanalazimika kununua tiketi kwa ‘mafungu’ kufuatia mtandao kusumbua kwenye kituo cha Kibaha Stendi.

“Huwa haijulikani ni muda gani mtandao utakuwa sawa, tunaambiwa twende Njuweni kukatia huko tiketi, kutoka Kibaha Stendi hadikituo cha Njuweni ambako kwa daladala nauli ni Sh 500 au Sh1000 kwa pikipiki ambayo ni gharama nyingine,”alisema.

Alisema kukitokea shida ya mtandao, abiria wanajikusanya na kulazimika kumuomba mwenye simu janja kuwanunulia tiketi, na wao kumlipa mtu huyo.

“Pale pale kituoni tunafanya hivyo, lakini ni usumbufu, ni lazima uwe na mtu huyo kuanzia mwanzo wa safari hadi unapofika stendi ya Kimara, ukimpoteza maana yake tiketi yako imepotea,” alisema.

Kero nyingine inaelezwa na Agripina Joackimu mkazi wa Kibaha alisema ni foleni kubwa wakati wa ununuzi wa tiketi.

"Nafikiri mabasi ni machache na hawataki kusema ukweli, mara nyingi tunajikuta tunachelewa kituoni kwa kusubiri basi kwa muda mrefu," alisema Agripina.

Kwa upande wa ununuzi wa tiketi, Hadija Rajabu mkazi wa Kibaha anashauri,

“Wangeiboresha huduma ya kununua tiketi kwa simu, labda ingesaidia kupunguza foleni ya tiketi, kwani hiyo huduma nayo ina siku na siku, kuna wakati unalipua, lakini hupati tiketi na hela wamechukua, ukilalamika ndio mwanzo wa kucheleweshewa muda, unajikuta unaamua kuingia gharama mara mbili," alisema.

Dart wajibu

Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, Mkuu wa Kitengo cha mawasiliano na uhusiano Dart, Willium Gatambi, alisema miongoni mwa sababu za kadhia hiyo ni mfumo wa kukatisha tiketi kusumbua.

“Wakati mwingine unachangiwa na kukatika kwa umeme,” alisema.

Kuhusu mabasi kutembea vituoni bila abiria, alisema ni kwa namna madereva wanavyopangiwa kufanya safari zao kwani kuna muda inabidi wakimbie eneo lingine ili kupunguza abiria kuwa wengi kituoni.

“Mabasi kupaki wakati vituoni kuna abiria, inatokana madereva wengine muda wao wa kufanya kazi kuwa umeisha hivyo wanabadilishana na wengine,” alisema.

Imeandikwa na Baraka Loshilaa, Imani Makongoro na Nasra Abdallah