Mwenge wa Uhuru wapitisha miradi yote wilayani Ludewa
Ludewa. Mbio za Mwenge wa Uhuru Wilayani Ludewa zilifanywa Aprili 25, 2023 na kuukabidhi wilayani Njombe jana Aprili 26, 2023.
Mwenge wa uhuru umekimbizwa kilometa 173 na kufanikiwa kupitia miradi 8 ndani ya Wilaya ya Ludewa yenye jumla ya thamani Sh2.24 bilioni.
Akizungumza kabla ya kukabidhi Mwenge wa Uhuru kwa Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Victoria Mwanziva amemshukuru Kiongozi wa Mbio za Mwenge Taifa na kuahidi kufanyia kazi yale yote waliyoelekezwa.
“ Namshukuru Mungu kwani huu ni Mwenge wangu wa kwanza, Pia nawashukuru viongozi wa mbio za Mwenge mwaka huu kwa ushirikiano wao mzuri, tumevuka salama na tumepokea maelekezo, maagizo yote ya miradi na tumepata ujumbe wa Mwenge wilayani Ludewa,” amesema Mwanziva.
Pia amewatakia kila la heri viongozi wa Wilaya ya Njombe katika kuukimbiza Mwenge wa Uhuru wilayani kwao.
Kwa upande wake Abdallah Shaibu Kaim ambaye ni Mkimbiza Mwenge Kitaifa ameupongeza uongozia wa Wilaya ya Ludewa kwa kuendelea kulinda mazingira.
“ Nawapongeza sana Ludewa inaendelea kuwa ya kijani kwa kweli mmeunga mkono dhima ya mwenge kwa mwaka huu 2023,” amesema.
Pia amewataka kudumisha upendo na ushirikiano katika kuendeleza kazi nzuri za kusimamia miradi.
“Naomba mwendeleze upendo baina yenu na ninawapongeza katika kazi nzuri za kusimamia miradi, muendelee kumsaidia Dkt. Samia,” amesema Kaim.