Mwenyekiti wa mtaa auwawa, mwili watupwa nje ya nyumba yake

Mwenyekiti wa mtaa auwawa, mwili watupwa nje ya nyumba yake

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Mtaa wa Hasanga Kata ya Uyole Jijini Mbeya, Justine Namwinga (47) ameuawa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia leo.

Mbeya. Mwenyekiti wa Mtaa wa Hasanga Kata ya Uyole Jijini Mbeya, Justine Namwinga (47) ameuawa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia leo Januari 31 na kisha mwili wake kutelekezwa nje ya nyumba yake.

Akizungumza katika eneo hilo, baba wa marehemu, Hance Mwashembele amesema awali alisikia jiwe likirushwa kwenye paa la nyumba yake, lakini hakutilia maanani, kwani alikuwa na usingizi.

''Nilisikia jiwe likirushwa juu ya bati usiku lakini sikutaka kufuatilia wala sikuwa na shaka na muda huo usingizi ulinipitia nikawa nimelala. Ilipofika alfajiri kuna mtoto wa jirani alikuja kunigongea mlango na kunitaka nitoke nje kwa maelezo mwanangu ameuawa nje ya nyumna,” amesema Mwashembele.

Amesema baada ya kutoa nje alimkuta marehemu akiwa amelala chini huku akiwa amefunikwa nguo.

Ameviomba vyombo vya usalama kusaidia kuchunguza tukio hilo, huku akisema marehemu ameacha watoto sita.

“Naomba Serikali inisaidie kwani sina la kusema mwanangu amekufa kweli walifanya mauaji haya naomba Serikali inisaidie ntaishije mimi,” amesema kwa uchungu.

Naye Mjumbe wa Nyumba 10, Tabia Mbilinyi amesema kuwa wameshtushwa sana na tukio hilo kwani marehemu alikuwa anafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na viongozi wenzie na hajawai kuwa na migogoro na mtu yoyote.

Kwa upande wake Mtendaji wa Mtaa huo, David Barton amesema kuwa kifo cha Mwenyekiti huyo ni pigo kubwa, hivyo wanaomba wananchi kushirikiana na vyombo vya bora kuwafichua watu waliohusiaka na tukio hilo na wanaojihusisha na matukio ya uharifu.



''Tunaomba wananchi kushirikiana na vyombo vya Dola kufichua watu walio husika na mauaji hayo ikiwa ni pamoja na kifichua waharifu kwani marehemu alikuwa mstari wa Mbele kupambana na uharifu,” amesema.

Barton ameongeza kuwa hivi karibuni kwa kushirikiana na marehemu katika ulinzi wa jadi sungusungu walifanikiwa kuokoa pikipiki iliyokuwa imeibiwa na vijana kutoka katika mtaa wa jirani hivyo watamuenzi kwa matendo makubwa ya kupigania haki za wanyonge.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Christian Musyani hakupatikana kuzungumzia tukio hilo kwa kile kilichoelezwa na msaidizi wake kuwa yuko kwenye kikao.