Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mazishi ya Ayatollah Khamenei yanasubiriwa kuandika upya kitabu cha Guinness

Muktasari:

  • Ilikuwa Juni 11, 1989, watu zaidi ya milioni 10.2, walihudhuria mazishi ya aliyekuwa Kiongozi Mkuu (Rahbar) wa Iran, Ayatollah Ruhollah Khomeini. Kitabu cha kumbukumbu za dunia cha Guinness, kilirekodi tukio hilo na rekodi hiyo imedumu kwa miaka 37.



Miaka 37 iliyopita, rekodi mpya ya dunia iliandikwa. Ilikuwa Juni 11, 1989, watu zaidi ya milioni 10.2, walihudhuria mazishi ya aliyekuwa Kiongozi Mkuu (Rahbar) wa Iran, Ayatollah Ruhollah Khomeini. Ilikuwa idadi kubwa zaidi ya watu kuhudhuria mazishi yoyote yale tangu dunia ilipoumbwa.

Kitabu cha kumbukumbu za dunia cha Guinness, kilirekodi tukio hilo, na rekodi hiyo imedumu kwa miaka 37. Sasa, mazishi ya Kiongozi Mkuu wa Iran, aliyeshika hatamu baada ya Ayatollah Khomeini, Ayatollah Ali Khamenei, yanakwenda kubadili maandishi ya kitabu cha Guinness, kwa jina la mhusika, na idadi ya wahudhuriaji, eneo la rekodi ni lile, ardhi ya Uajemi, Iran.

Ile siku, Juni 11,1989, ilikuwa Jumapili, msululu wa watu ulitanda kwenye jiji la Tehran, kuelekea makaburi ya Behesht-e Zahra. Eneo ambalo watu walifurika kumzika Ayatollah Khamenei, lilikadiriwa kuwa na ukubwa wa kilometa 32. Kwa vipimo vya Dar es Salaam, ni sawa na watu kupanga foleni kwa mamilioni kutoka Posta (katikati ya jiji), mpaka Bunju, au Kariakoo hadi Kibaha, Pwani.

Mwaka 1989, idadi ya watu Iran ilikuwa milioni 56.7. Hivyo, kwa watu milioni 10.2 kuhudhuria mazishi, maana yake asilimia 18, ya watu wote wa nchi hiyo kwa wakati huo, walishiriki mazishi ya aliyekuwa kiongozi wao, Ayatollah Khomeini. Kwa mwaka 1989, idadi ya wakazi wa Tehran walikuwa milioni sita tu.  Wananchi wa Iran walisafiri kutoka miji mbalimbali, na kukutana Tehran, kumzika Khomeini.

Sababu ya mahudhurio makubwa ya mazishi ya Khomeini, ni mbili kubwa; kwanza Khomeini hakuwa tu mkuu wa nchi, bali pia kiongozi wa kidini. Asilimia 90 mpaka 95 ya Wairan ni Waislam madhehebu ya Shia. Ayatollah Komeini alitazamwa kama mkuu wa Shia ulimwenguni. Hivyo, kulikuwa na nguvu ya mvuto wa kiroho.

Pili, Khomeini, kwa kuongoza Mapinduzi ya Iran mwaka 1979, na kuanzisha Jamhuri ya Kiislam ya Iran, alisherehekewa na Wairan kama kiongozi aliyekomesha uvamizi wa mataifa ya kigeni kwenye nchi yao. Kwa Wairan, Khomeini alibeba alama ya ushujaa dhidi ya Uingereza na Marekani, ambao walikuwa wakichota mafuta ya Iran walivyotaka kabla ya mapinduzi ya mwaka 1979.

Khomeini, alifariki dunia Juni 3, 1989, akiwa na umri wa miaka 89. Sababu ya kifo chake ilikuwa kuvuja damu kwenye mfumo wake wa mmeng’enyo wa chakula. Ndani ya siku 10 za mwisho za uhai wake, Khomeini alipata mashambulizi matano ya moyo, lakini alinusurika. Alifia kwenye Hospitali ya Jamaran, Tehran.

Kifo cha Khomeini kilitikisa dunia. Pakistan ilitangaza siku 10 za maombolezo. Syria iliomboleza kwa siku saba. Afghanistan, Lebanon, na India, zilirusha bendera nusu mlingoti kwa siku tatu. Kwa kifupi, mahudhurio ya mazishi ya Khomeini, yaliandika rekodi ya mkusanyiko mkubwa zaidi wa watu kwa wakati mmoja, katika historia ya dunia.

Watu nane walifariki dunia kwa sababu ya msongamano. Zaidi ya watu 500 walijeruhiwa. Kutokana na idadi kubwa ya watu, ilishindikana kuusafirisha mwili wa Ayatollah Khomeini kwa gari, maana barabara hazikupitika. Ililazimu serikali kutumia helikopta ya Jeshi la Anga la Iran (IRIAA), aina ya Bell 214A/C, ambayo ndiyo iliubeba mwili wa Khomeini kutoka msikikiti wa Ayatollah Mkuu Mohammad-Reza Golpaygani, ulikosaliwa sala ya maiti, hadi makaburi ya Behesht-e Zahra, ulipozikwa.


Rekodi ya Khamenei

Julai 3, 2026, Ijumaa, shughuli za mazishi ya Ayatollah Khamenei zilianza. Februari 28, 2026, Khamenei aliuawa kwa mashambulizi ya makombora, yaliyoelekezwa kwenye makazi yake, jijini Tehran. Watu wengine saba, miongoni mwao wakiwa wasaidizi wake, pamoja na wanafamilia wake, nao waliuawa kwenye mashambulizi hayo yaliyotekelezwa kwa ushirikiano wa Marekani na Israel.

Awali, mazishi ya Ayatollah Khamenei, yalikuwa yafanyike Machi. Yalisogezwa mbele kwa sababu ya vita ya Iran dhidi ya Marekani na Israel, iliyokuwa ikiendelea. Kilele cha mazishi ya Khamenei, kitakuwa Julai 10, 2026, kwenye makaburi ya msikiti wa Imam Reza, mjini Mashhad. Khamenei atazikwa hapo kwa sababu kiimani, alikufa shahidi, yaani aliuawa akipigania dini.

Mashhad, kwa lugha za Kiajemi na Kiarabu, ni neno lenye maana ya eneo la mashahidi, au eneo la watu waliokufa mashahidi. Mji huo ndipo lilipo kaburi la Imam Ali al-Rida (Imam Reza), ambaye ni Imam wa Nane wa Shia. Ali aliuawa kwa sumu Juni 6, 818, hivyo naye alikufa shahidi. Hiyo ndiyo sababu ya jiji hilo kuitwa Mashhad. Na ndiyo mji mtakatifu namba moja Iran, kwa imani ya Shia. Mashhad pia ndipo alipozaliwa Ayatollah Khamenei.

Tangazo la Serikali ya Iran, limeweka makisio kuwa watu zaidi ya milioni 20 watahudhuria mazishi ya Khamenei. Maana yake ni kwamba itakuwa mara mbili ya mahudhurio ya Khomeini miaka 37 iliyopita. Kwa hesabu hiyo, kikokotoo ni kwamba asilimia 21 ya wananchi wa Iran, wanatarajiwa kuhudhuria mazishi ya kiongozi wao. Kwa sasa, idadi ya watu Iran ni milioni 93.2. Hii ni kwa mujibu wa mtandao wa takwimu duniani wa Woldometer.

Mji wa Mashad una wakazi milioni 3.4, na Tehran kwa sasa ni milioni 9.6. Mji mwingine wenye watu wengi ni Isfahan, ambao watu wake ni milioni 2.3. Ukitazama idadi hiyo, maana yake mamilioni ya watu watasafiri kutoka kona mbalimbali za nchi hiyo, kuelekea Mashhad, ili kuhudhuria maziko ya Ayatollah Khamenei.

Ijumaa, Julai 3, 2026, ambayo ilikuwa siku ya kwanza ya ratiba ya mazishi, jeneza lenye mwili wa Ayatollah Khamenei, liliwekwa kwenye ukumbi wa Imam Khomeini (Imam Khomeini Grand Mosalla), ambao ulijengwa maalum kwa ajili ya kufanyia ibada za halaiki, pamoja na kufanyia matukio mengine ya kidini, kijamii, na kiserikali, yenye kuhusisha idadi kubwa ya watu.

Katika ukumbi wa Imam Khomeini, Tehran, jeneza lenye mwili wa Ayatollah Khamenei, liliwekwa kwenye jukwaa, pamoja na majeneza yenye mabaki ya miili ya watu wa familia yake, waliouawa pamoja naye Februari 28, 2026. Viongozi kutoka nchi zaidi ya 100 duniani, walishiriki ibada ya mazishi ya Khamenei. Hii ni kwa mujibu wa Shirika la Habari la Iran, IRIB.

Julai 4 na 5, 2026 (Jumamosi na Jumapili), ilikuwa siku ya mahudhurio ya umma, kwenye ukumbi wa Imam Khomeini, jijini Tehran. Julai 6 na 7, 2026 (Jumatatu na Jumanne), jeneza la mwili wa Ayatollah Khamenei liliwekwa hadharani kwenye jiji la Qom. Watu takriban milioni 5, wa wamekadiriwa kuhudhuria ibada ya dua ya kumuaga Ayatollah Kahamenei.

Idadi ya wakazi wa Qom ni milioni 1.5. Hiyo ina maana kuwa watu milioni 5 walioshiriki dua ya Ayatollah Khamenei, walisafiri kutoka maeneo mbalimbali. Inatoa tafsiri kwamba kila mwili unaposafirishwa kwenda kituo kingine, watu walisafiri kuufuata ili kuhakikisha wanatii kiu yao ya kumuaga kiongozi wao kwa miaka 45. Miaka nane akiwa Rais, miaka 37, akiwa Kiongozi Mkuu wa taifa lao.

Mamlaka za Tehran, zilichagua kuupeleka mwili wa Khamenei kwenye jiji la Qom, kwa sababu ni mji mtakatifu kwa imani ya madhehebu ya Shia. Qom ndipo lilipo kaburi la Fatma Masumeh, ambaye ni mchamungu wa daraja la juu kwa muongozo wa Shia. Fatima ni binti wa Imam wa Saba wa Shia, Musa al-Kazim, na alikufa mwaka 816.

Kwa kitendo cha Qom kuhifadhi kaburi la Fatima Masumeh (Fatima binti Musa), umepewa hadhi ya kuwa mji mtakatifu namba mbili baada ya Mashhad. Fatima pia ni dada wa Imam Reza, Imam wa Nane wa Shia, ambaye kaburi lake lililopo Mashhad, ndiyo sababu ya mji huo kuwa na utakatifu namba moja.

Julai 8 na 9, 2026 (Jumatano na Alhamisi), mwili wa Ayatollah Khamenei utapelekwa Iraq, kwenye majiji ya Najaf na Karbala. Jumatano, mwili utapokelewa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Najaf, Iraq, kisha dua ya umma itasomwa Najaf, halafu Alhamisi itakuwa zamu ya Karbala.

Mwili wa Ayatollah Khamenei unapelekwa Najaf na Karbala kwa sababu kwa Shia, miji hiyo ni mitakatifu. Najaf, ndipo alipouawa na kuzikwa binamu wa Mtume Muhammad (S.A.W), Ali bin Abi Twalib mwaka 661. Ali ni Khalifa wa Nne, yaani kiongozi wa nne wa Uislam duniani, tangu kifo cha Mtume Muhammad. Imam Ali pia alimwoa Fatma, binti wa mwisho wa Mtume Muhammad.

Kwa madhebu ya Shia, Ali ni Imam wa Kwanza. Ndiye kitovu cha madhehebu yao. Hivyo, mwili wa Khamenei unapitishwa na kuombewa dua Najaf lilipo kaburi la Imam Ali, ili kupata baraka za kiongozi wa umma wao, kisha Karbala, yalipo makaburi ya Imam Hussein na Imam Abbas, ambao ni watoto wa Imam Ali, vilevile wajukuu wa Mtume Muhammad. Hussein na Abbas waliuongoza umma kwa vipindi tofauti baada ya kifo cha baba yao.

Ijumaa, Julai 10, 2026, mwili wa Ayatollah Khamenei, utafikishwa Mashhad, kwa ajili ya shughuli ya maziko. Endapo hesabu ya watu zaidi ya milioni 20 itafikiwa au kuzidi, maana yake, mazishi ya Khamenei yatakwenda kuhariri maandishi ya kitabu cha kumbukumbu za dunia cha Guinness, kwa kuweka rekodi ya mpya ya ulimwengu na kuongoza kwa kuwa mkusanyiko mkubwa zaidi wa watu kuwahi kutokea duniani.