Mwigulu amuibua msanii, aagiza aingizwe kwenye ziara zake akatumbuize
Kijana mkazi wa Mabogini, Wilaya ya Moshi akitumbuiza kwenye moja ya ziara ya Waziri Mkuu, eneo la stendi ya mabasi ya Kimataifa ya Ngangamfumuni Manispaa ya Moshi.
Muktasari:
- Awali kijana huyo, alimweleza Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba kwamba anao uwezo mkubwa wa kuimba lakini hajulikani licha ya kwamba kijiji kizima kinamfahamu.
Moshi. Kijana mkazi wa Mabogini, Wilaya ya Moshi, amejikuta akipata fursa ya kipekee baada ya kuvutia umati na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, kwa kipaji chake cha kuimba katika mkutano wa hadhara.
Tukio hilo lilitokea Februari 20, 2026 katika Kata ya Mabogini, ambapo kijana huyo aliomba nafasi ya kuwasilisha kero zake mbele ya Waziri Mkuu. Mbali na kuzungumzia changamoto mbalimbali ikiwemo ya huduma za afya, alitumia jukwaa hilo kueleza ndoto yake ya muziki.
“Kingine Mheshimiwa, mimi ni msanii, naimba. Kijiji chote wanajua naimba lakini sijulikani, naona kama naimbia nyumbani tu,” alisema kijana huyo huku akishangiliwa na baadhi ya wananchi.
Baada ya kauli hiyo, Dk Mwigulu alimpa nafasi ya kuonesha kipaji chake kwa kuimba sehemu ya wimbo wake unaoitwa Ukifika kwetu jionee.
Akiwa jukwaani, kijana huyo aliimba:
“Ukifika kwetu jionee… Mkoa wa Kilimanjaro muonee, ukifika kwetu pale Moshi Mjini ulizia Soko la Mbuyuni… ukishuka chini wanapaita Manyema, vitu bei bei poa tu… kuuza leshuu kazi inaendelea, kuuza vitunguu kazi inaendelea…”
Uimbaji huo uliibua shangwe kutoka kwa mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano huo, wakimpigia makofi na kushangilia kwa furaha.
Baada ya kusikiliza wimbo huo, Dk Mwigulu alimpongeza kijana huyo kwa kipaji chake na kuagiza aingizwe kwenye msafara wake wa ziara ili awe akitoa burudani katika mikutano ya hadhara.
“Mbona unaweza bhana! Katibu, huyu awepo kwenye msafara aburudishe kila mkutano. Hebu muwekeni kwenye msafara… ee bhana si unaona? Mchukueni kule,” amesema Dk Mwigulu huku akielekeza maofisa wake.
Hatua hiyo ilizua nderemo na vifijo kutoka kwa wananchi, huku kijana huyo akionekana kuguswa na uamuzi huo.
Akizungumza baada ya tukio hilo, kijana huyo alimshukuru Waziri Mkuu kwa kumtambua na kumpa fursa ya kuonesha kipaji chake mbele ya hadhira kubwa, akisema ni mwanzo mpya wa safari yake ya muziki.