Mwili wa kijana mwenye ualbino wakutwa shambani Morogoro

Kijana Rashid Mussa (24) enzi za uhai wake.
Muktasari:
- Mwili wa kijana mwenye ualbino, Rashid Mussa (24), umekutwa shambani baada ya kutoweka kwa siku tatu.
Morogoro. Mwili wa kijana mwenye ualbino, Rashid Mussa (24), umekutwa katika shamba la mtu asiyejulikana, baada ya kutoweka nyumbani kwake kwa siku tatu.
Rashid alitoweka kutoka kijiji cha Kiziwa, Kata ya Kiroka, wilaya ya Morogoro, na mwili wake ulipatikana kwenye shamba hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama, amesema leo Ijumaa, Januari 17, 2025 kuwa uchunguzi wa awali umeonyesha chanzo cha kifo hicho ni kuanguka kutoka juu ya mnazi aliokuwa akiupanda.
Kaka wa marehemu, Juma Kibwana, maarufu Bonge, amesema alipata taarifa kutoka kwa wasamaria wema kuhusu mwili wa mdogo wake, uliokutwa pembeni ya mti wa muembe, jirani na mnazi.
Kibwana amesema waliona nazi 14, kamba ya kupandia mnazi na panga.
Amesema mwili ulikutwa ukiwa umeharibika.
“Baada ya uchunguzi wa daktari, walikabidhi mwili kwa familia na tukazika," amesema Kibwana.
Mama mzazi wa marehemu, Zawadi Fundi, ambaye pia ni mlemavu wa viungo, amesema aligundua kutoweka kwa mtoto wake asubuhi ya Januari 13, 2025 baada ya kuona mlango wa chumba alicholala ulikuwa umefungwa na kufuli, jambo ambalo halikuwa la kawaida.
"Sikuwa na uwezo wa kwenda kumtafuta mwenyewe kwa sababu ya ulemavu wangu. Nilimwambia ndugu zake waende kumtafuta, mwishowe walikuta mwili wake," amesema.
Amesema Rashid alikuwa tegemeo katika familia kutokana na hali yake ya ulemavu na ugumu wa maisha.
Habiba Fundi, mama mdogo wa marehemu, amesema hakuwahi kusikia iwapo kijana wao alikuwa akihusika na vitendo vya wizi au ugomvi na mtu yeyote.
Kamanda Mkama amesema polisi wanaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini undani wa tukio hilo.