Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Albino auawa, wawili wakatwa viungo (2)

Baba mzazi wa marehemu Lugolola (7), Bunzari Shinga akiwa na majeraha aliyopata wakati akijaribu kumwokoa mtoto wake alipovamiwa na majambazi.

Muktasari:

“Ile kutoka tu, nilikumbana na risasi tatu tumboni na moja ilinipitia mguu wa kulia na kunitengua nguvu za kuendelea kusimama.  Nilianguka na kulala kwenye vumbi kwa muda.  Walipoona sitikisiki waliniacha palepale na kuendelea na uovu wao,”

Jana tuliishia pale Gama alipo zinduka na kujikuta akiwa katika Wodi ya Wanawake ya Hospitali ya Kitete na kueleza masikitiko yake ya kufiwa na mjukuu wake na baba yake mzazi ambao licha ya kuuawa bila ya hatia, hakupata hata fursa ya kuwaaga na kuwazika.

GAMA anaeleza kwamba miezi michache iliyopita, familia ilikuwa imepanga kumpeleka Lugolola kwenye Shule ya bweni baada ya kusikia taarifa za kuuawa na kukatwa viungo kwa watu wenye ulemavu wa ngozi.

“Lakini tukaambiwa kwamba umri wake ni mdogo kwa shule ya bweni. Hivi hawa watu walikuwa wanasubiri hadi mwana ngu auawe? Hii ni kazi ya ndani tu. Hakuna mtu wa nje ambaye angeweza kujua mahali aliko Lugolola, ambaye alikuwa amelala kama siyo jirani au ndugu wa familia hii,” anasema mmoja wa ndugu wa familia aliyejitambulisha kwa jina la John.

Usiku ule wa mauaji Bunzari, aliposikia vilio vya watoto alitoka nje ya nyumba ya pili na kuelekea kwenye nyumba ya Babu Zengabuyanda.  

“Ile kutoka tu, nilikumbana na risasi tatu tumboni na moja ilinipitia mguu wa kulia na kunitengua nguvu za kuendelea kusimama.  Nilianguka na kulala kwenye vumbi kwa muda.  Walipoona sitikisiki waliniacha palepale na kuendelea na uovu wao,” anasimulia Bunzari akiwa katika Wodi ya Wanaume katika Hospitali ya Kitete.

“Nilipoona kuwa wameniacha, nilitambaa hadi kwenye shamba la mahindi na kuelekea msituni. Wakati nilipokuwa kule nikasikia sauti ya babu akitutahadharisha kwamba kaya yetu imevamiwa.”

“Watoto waliendelea kulia na huku nikisikia jinsi majambazi hao yalivyokuwa yakiwachapa watoto kwa fimbo. Baadaye nilisikia sauti ya mwanangu mpenzi Lugolola.”

“Alilia  kwa uchungu na kutoa sauti kubwa mara moja tu na kisha sikumsikia tena. Ilikuwa kama uwanja wa vita. Hawa wali dhamiria kuua kila mtu ili wapate mkono wa mwanangu!  Hivi amewakosea nini?”  alisema Bunzari huku akilia... na kuongeza:  “Babu yangu mpenzi amewakosea nini watu hawa?”

Muuguzi alisema risasi tatu zilitolewa kwenye nyonga na kwamba hali yake ilikuwa inaendelea vizuri.

Mke mdogo wa Bunzari, Pili, aliniambia kuwa aliposikia risasi zikirindima na nyingine kupiga ukutani, alijificha chumbani mwao hadi alipohisi kuwa majambazi yameondoka.

“Nilimbeba mwanangu na kukimbilia msituni nikimwita mume wangu kwa jina. Nilimkuta mtoto mmoja amekaa karibu naye. “Akamwambia kuwa ati akifariki dunia kwa kuwa alikuwa anatoka damu nyingi, basi yule mtoto awaelekeze watu kule msituni ili wamuokote na kumzika asiozee msituni. Nilimsaidia Bunzari hadi kwa jirani umbali wa kilomita moja hivi,” anasema Pili.  

Bunzari alipakiwa kwenye pikipiki na kupelekwa Zahanati ya Kanoge, kilomita 15 hivi kutoka nyumbani kwake ambako alipatiwa huduma ya kwanza na baadaye alipelekwa Tabora kwa gari la polisi.

Mtu ambaye hakuguswa na silaha hata kidogo ni Kulwa, mke wa kwanza wa Bunzari na ambaye ni mama mzazi wa Lugolola.

Huku akiendelea kumenya maharage mabichi alinisimulia jinsi alivyowatoa watoto wake aliokuwa nao usiku huo wakati wauaji hao wakiwa nje ya nyumba yake.  

“Niliposikia kelele za watoto kutoka nyumbani kwa babu niliamka na kutoka nje. Nilipofika mlangoni nikawaona watu wanne wenye silaha za mapanga, magobole na marungu nje ya nyumba yangu.”

“Mbele ya mlango wa babu niliwaona watu watatu pia wakiwa na silaha. Mtu mwingine mwenye silaha ikiwamo gobole alisimama mbele ya nyumba ya pili. Nilirudi ndani na kumchukua Shija, dada yake Lugolola na huyu wa mgo ngoni nikawapeleka vichakani. Nikarudi nikamchukua mdogo wake Lugolola mwenye miaka mitatu na kumpeleka vichakani.”

“Nilipokuwa huko nikasikia sauti ya Lugolola ikilia mara moja tu. Kisha kukawa na kimya kikuu. Niliporudi nyumbani ndipo nikamkuta mwanangu ame nyofolewa mkono na amekufa.”
Hakuonyesha simanzi wala hakuzungumza kwa uchungu.  Kwangu mimi kama mzazi, iliniwia vigumu kumwelewa Kulwa. Kwanza nikiiangalia hali nzima ya mashambulizi katika kaya hiyo nikagundua kwamba yeye peke yake kati ya watu wote wazima hakuguswa hata kidogo na wauaji hao.

Amekutana nao ana kwa ana mara tatu na hakuna kilichomtokea. Kisha aliingia mara mbili ndani ya nyumba yake na kuwachukua watoto wale wengine wasio na albino na kuwaficha vichakani bila kukumbana na hasira za wauaji.

Swali nililomwuliza na ambalo hakulijibu ni kwa nini mara ya kwanza alipoingia ndani haku mchukua Lugolola mwenye umri wa miaka saba na ambaye anatembea mwenyewe bila kubebwa?
Iweje alimwacha mwanaye mwenye matatizo ya albino chumbani wakati anaingia na kutoka kuwasalimisha wengine?

Zengabuyanda Meli alishambuliwa na kuuawa mara tu alipotoka nyumbani kwake kwa lengo la kumwokoa Lugolola. Naye Gama Zengabuyanda alishambuliwa kwa mapanga alipojaribu kwenda walikolala watoto aliposikia vilio vyao. Bunzari alipigwa risasi nne na nyingine nne zikafikia ukutani alipotoka tu ndani ya nyumba yake.  

“Mama Lugolola, imekuwaje wewe hukuguswa? Nilimwuliza Kulwa. “Sijui sasa!”  lilikuwa jibu lake.
Bado nikiwa katika kaya hiyo ya Bunzari, maofisa wa polisi baadhi yao wakiwa na silaha waliwasili. Tulisalimiana na kujitambulisha na kisha walitaka niwapishe waendelee na uchunguzi wao.

Nilitumia muda huo kuzungumza na baadhi ya ndugu na jamaa waliokuwa pale. Karibu wote walisisitiza kwamba lazima kuna mtu wa karibu sana na familia au mwana familia ambaye alifanya njama hizo za kuuawa kwa Lugolola.  Niliwasihi watoe taarifa hizo kwa siri kwa polisi ili wahusika wakamatwe.

Nilifika kwenye kaburi la Lugolola lililokuwa pembeni mwa zizi lakini mbali na lile la ndugu yake Maganga. Yote mawili yalikuwa ni ya udongo tu. Nilimwuliza Kulwa kwa nini Lugolola hakuzikwa karibu na mdogo wake aliyefariki kwa malaria.

“Familia imeamua hivyo!” ndilo lilikuwa jibu lake. Nilitaka kujua kama watalijengea kwa kutumia nondo, matofali na zege ili kuzuia watu wasije wakachukua viungo vilivyobaki.  Makaburi mengi ya albino huimarishwa hivyo ili viungo vyao visitolewe na kupelekwa kwa waganga wa kienyeji.   

Itaendelea kesho...