Mwili wa Magufuli kuagwa mikoa minne

Mwili wa Magufuli kuagwa mikoa minne

Muktasari:

  • Msemaji wa Serikali ya Tanzania, Dk Hassan Abbas amesema ratiba ya mazishi ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli imekamilika na itatolewa kwa umma leo Ijumaa Machi 19, 2021 na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.

Dar es Salaam. Msemaji wa Serikali ya Tanzania, Dk Hassan Abbas amesema ratiba ya mazishi ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli imekamilika na itatolewa kwa umma leo Ijumaa Machi 19, 2021 na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.

Akizungumzia maandalizi ya ratiba Dk Abbas amesema mwili wa Magufuli utaagwa Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Geita na Chato ambako utazikwa.

“Kama nilivyosema kumekuwa na vikao vingi, ratiba imekamilika kwa hiyo tutarajie makamu wa Rais atatoa taarifa kwa umma kuhusu ratiba na mtiririko mzima wa maziko.”

“Kiufupi shughuli zitaanzia Dar es Salaam, wananchi wa Dodoma watapata fursa ya kuaga, pia wa  Mwanza nao, Geita na Chato atakapozikwa. Kuhusu tarehe atakayozikwa na utaratibu utakavyokuwa makamu wa rais ataitangaza,” amesema Abbas.

Amesema katika utaratibu huo itaelezwa barabara ambazo mwili utapita, viwanja vutakavyotumika na kuwaomba wananchi kuajindaa kumuaga kiongozi huyo aliyefariki dunia Machi 17, 2021 kwa ugonjwa wa moyo baada ya kulazwa tangu Machi 6, 2021.

Wakati Dk Abbas akieleza hayo, leo saa 4 asubuhi itafanyika hafla fupi ya Samia mkuapishwa kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na huenda baada ya kiapo hicho akaeleza taratibu za mazishi ya Magufuli.