Mwili wa Magufuli wawasili Chato, wananchi watandika kanga barabarani
Muktasari:
- Vilio, wananchi kutandika kanga barabara na kulala ni kati ya mambo yaliyojitokeza wilayani Chato Mkoa wa Geita wakati mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, marehemu John Magufuli ukiwasili wilayani humo leo jioni Jumatano Machi 24, 2021.
Dar es Salaam. Vilio, wananchi kutandika kanga barabara na kulala ni kati ya mambo yaliyojitokeza wilayani Chato Mkoa wa Geita wakati mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, marehemu John Magufuli ukiwasili wilayani humo leo jioni Jumatano Machi 24, 2021.
Wakazi wa Wilaya hiyo ambako ndio yatafanyika maziko ya Magufuli wamejitokeza barabarani na kupunga mkono huku wakiimba na kuomba na wengine wakisema “jeshi, jeshi, jeshi” kama ishara ya heshima kwa kiongozi huyo aliyefariki dunia Machi 17, 2021.
Baadhi ya maeneo ya mji huo yamebandikwa mabango yenye ujumbe mbalimbali, pumzika shujaa wa Afrika, baba yetu mwadilifu wana Chato tunakulilia daima tutakuenzi, pumzika kwa amani shujaa wa Afrika.
“Mwamba alizoea kuja lakini sasa mwamba amelala,” walisikika wakisema baadhi ya waombolezaji waliokuwa wamejipanga barabarani.
Awali, kabla ya mwili kuwasili walitandika kanga katika mitaa mbalimbali ambayo mwili huo utapita.
“Tumeumia sana kwa mengi aliyotufanyia Chato.
Naumia sana moyoni kwa sababu kiongozi wangu ameondoka, hapa kazi ni nyingine lakini tunashukuru aliyepo atatupeleka pazuri tunaamini hivyo.”
“Msiba huu umenigusa sana moyoni ninasikia maumivu makali, akija kututembelea tunapata fursa za kuuza vitu, vitu alivyoviwekeza ndiyo alama yetu na nitazidi kumuita Rais wangu sitaita marehemu, nina huzuni kubwa sana kumpoteza rais wangu alitufanyia mazuri makubwa mpaka sasa Tanzania nzima tuna huzuni kubwa ninaomba Mungu amlaze pema peponi,” amesisitiza mmoja wa wananchi.