Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwili wa Moreen wasafirishwa Chato kwa mazishi

Muktasari:

  • Mwili wa mtoto Moreen Nyamajeje (9), mwanafunzi wa darasa la tatu aliyedaiwa kunyongwa hadi kufa na watu wasiojulikana Mtwara, umesafirishwa kwenda Wilaya ya Chato mkoani Geita kwa ajili ya mazishi, huku familia yake ikiondoka Mtwara na wakazi wa eneo hilo wakiendelea kuishi kwa hofu.

Mtwara. Mwili wa mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi King David, Moreen Nyamajeje (9), anayedaiwa kunyongwa hadi kufa na watu wasiojulikana, umesafirishwa kwenda Wilaya ya Chato, Mkoa wa Geita kwa ajili ya mazishi.

Moreen anadaiwa kuuawa Juni 21, 2026, majira ya saa 11 jioni, alipokuwa akicheza na watoto wenzake nje ya nyumba yao iliyopo katika Kambi ya Jeshi la Magereza Lilungu, Manispaa ya Mtwara Mikindani.

Inadaiwa mtu asiyejulikana aliwaita watoto hao mmoja baada ya mwingine kwa ishara kabla ya kumchukua Moreen na kwenda naye katika shamba la Magereza, ambako alidaiwa kumnyonga hadi kufa.

Akizungumzia kuagwa kwa mwili wa mtoto huyo, Mwenyekiti wa Wanawake katika Kambi ya Jeshi la Magereza Lilungu, Jasmini Abdallah amesema mwili uliagwa jioni Juni 22, 2026 na kusafirishwa kwenda Chato kwa ajili ya mazishi.

“Tumeaga mwili wa mtoto jana, na jana hiyo hiyo uliondoka baada ya kuagwa majira ya saa 12 jioni. Hakuna aliyebaki kwenye nyumba yao; mama wa marehemu na mtoto mmoja aliyebaki wote wameondoka. Nyumba imefungwa, hakuna familia iliyobaki pale,” amesema Jasmini.

Amesema wakati tukio hilo linatokea, baba wa marehemu alikuwa Chato alikokwenda kuhudhuria mazishi ya ndugu yake.

“Mama wa marehemu alikuwa na watoto wawili akiwemo marehemu na mwingine aliyebaki. Baba wa marehemu hakuwepo, alikuwa safarini. Alienda kuzika kwao baada ya kufiwa na mama yake mdogo.

“Siku ya tukio la mwanawe ndipo walikuwa wanainua tanga ili aanze safari ya kurudi, ndipo akapata taarifa za kifo cha mwanawe. Wazee wa ofisi wakamshauri asirudi kwa sababu gharama zingekuwa kubwa, wamwambie abaki huko huku wao wakisimamia taratibu zote Mtwara,” amesema.

Jasmini amesema tukio hilo limewaacha wakazi wa kambi hiyo wakiwa na majonzi na hofu kubwa.

“Sisi ni wananchi tunaoishi kambini, kwa hiyo hili tukio lililotokea ni la kinyama. Kila mtu amekuwa muoga, wakati kambini ni sehemu yenye ulinzi mkubwa, lakini limetokea tukio hili la kikatili,” amesema.

Naye mkazi wa kambi hiyo, Rusiana Ally, amesema jamii inaendelea kuishi kwa hofu kufuatia tukio hilo ambalo hawakulitarajia.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Lilungu, Fatuma Ally, amethibitisha kuagwa kwa mwili wa mtoto huyo Juni 22, 2026 na kusafirishwa kwenda Chato kwa mazishi, akisema bado familia haijathibitisha rasmi siku ya mazishi, huku mawasiliano yakiendelea.