Mwingine ashindwa kufanya mtihani la saba, adaiwa kuchomwa moto na mama yake

Muktasari:

  • Baada ya jana kuripotiwa kuuawa mwanafunzi wa darasa la saba, Farida Makuya wa Shule ya Msingi Mtumba, Dodoma mwanafunzi mwingine wa darasa hilo, Hellena Paulo wa Shule ya Msingi Shahende mkoani Geita amechomwa moto na mtu anayedaiwa ni mama yake na hivyo kushindwa kufanya mitihani yake.


Geita. Baada ya jana kuripotiwa kuuawa mwanafunzi wa darasa la saba, Farida Makuya wa Shule ya Msingi Mtumba, Dodoma mwanafunzi mwingine wa darasa hilo, Hellena Paulo wa Shule ya Msingi Shahende mkoani Geita amechomwa moto na mtu anayedaiwa ni mama yake na hivyo kushindwa kufanya mitihani yake.

Kwa mujibu wa mwalimu mkuu wa shule hiyo, Holela Emanuel amedai tukio hilo limetokea Oktoba 3, 2022.

Amedai sababu ya tukio hilo ni mama huyo kumuadhibu kwa kumchoma moto mtoto huyo, baada ya mzazi huyo kudai mtoto wake amemsaliti kwa kumueleza mwalimu kuwa ameambiwa asifanye vizuri kwenye mitihani ili asifaulu.

Mwanafunzi huyo ambaye alipaswa kufanya mtihani wa darasa la saba kuanzia jana na kumaliza leo, amejikuta akishindwa kufanya mitihani hiyo.

Mwalimu Emanuel amesema mwanafunzi huyo alifika shuleni Jumatatu na kuosha dawati na Jumanne ikiwa ni siku moja kabla ya kuanza mtihani wa Taifa, walipaswa kurudi shuleni kupewa namba ya mtihani lakini yeye hakufika.

“Nilimtuma mwanafunzi mwingine ambaye ni ndugu yake amwambie afike shuleni siku ya Jumatano kwa ajili ya mtihani bila kukosa.

 “Kweli asubuhi alikuja na kwa kuwa kuna utaratibu wa kunawa mikono alishindwa kunawa nilipomhoji kwa nini hanawi alinionyesha mikono ikiwa imevimba na mguu wake ukiwa umetobolewa na kitu na nipomchunguza sababu alidai mama yake amempiga kwa kudai amemsaliti kwa kukubali kufaulu mtihani,” amesema

Amesema mwanafunzi huyo ni miongoni mwa wanafunzi waliotegemewa kufaulu mtihani kutokana na juhudi zake darasani.

Mwalimu amesema katika kijiji hicho cha Butobela mkoani Geita changamoto ya wazazi kuwarubuni wanafunzi kipindi cha mitihani ili wasifanye vizuri kwenye mitihani yao ya mwisho ili waweze kuwasaidia kwenye shughuli za kiuchumi.

“Kilichotokea hapa mama alipokamatwa amewaeleza polisi kuwa mtoto aliiba Sh30,000 lakini huyu mama ni familia duni sana hapa kijijini hawezi kuweka 30,000 ndani na hili sio tukio la kwanza yupo pia mtoto wa kiume alimwadhibu na alipokamatwa alidai amemuibia, amekuwa akitumia hii kama mbinu tuu” amedai mwalimu

Mjomba wa mtoto huyo akizungumza kwa niaba ya familia ya Mabula Nyaruru amedai kitendo kilichofanywa na dada yake Manyamizi Nyaruru ni cha kinyama lakini kinatokana na hali ngumu ya maisha anayoishi mama huyo.

Amedai dada yake anawatoto watano aliozaa na wanaume watano tofauti na anawalea mwenyewe.

Akizungumzia kiasi cha fedha kilichoibiwa amedai dada yake alidai mtoto huyo ameiba Sh1000.

Naye, afisa elimu Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Edith Mpinzile amethibitisha mwanafunzi huyo kushindwa kufanya mtihani kutokana na mzazi wake kumjeruhi mikono kwa moto.

“Ni kweli mtoto hajafanya mtihani na tunachofanya ni kumsaidia ili aweze kufanya mtihani mwakani huyu, sasa ameshindwa kutokana na tukio alilofanyiwa wapo wengine hawajafanya kutokana na utoro bado tunakusanya takwimu “amesema Mpinzile

Afisa mtendaji wa kijiji cha Butobela Edar Michael amesema taarifa za mtoto huyo kutofanya mtihani zilitolewa na mwalimu mkuu na walipofuatilia walimkuta mtoto amejeruhiwa maeneo ya mikono yote miwili.

Mwanafunzi huyo amepatiwa matibabu kwenye kituo cha afya Bukoli na mama anashikiliwa na Jeshi la Polisi katika kituo kidogo cha Bukoli.