Mwita Dar azuiwa kushiriki vikao baraza la madiwani

Muktasari:

Meya wa Jiji la Dar es Salaam aliyeng'olewa, Isaya Mwita amezuiwa kushiriki kikao cha kamati za huduma za jamii za baraza la madiwani la Jiji la Dar es Salaam na cha kamati ya  mipango miji, mazingira na usafirishaji.

Dar es Salaam. Meya wa Jiji la Dar es Salaam aliyeng'olewa, Isaya Mwita amezuiwa kushiriki kikao cha kamati za huduma za jamii za baraza la madiwani la Jiji la Dar es Salaam na cha kamati ya  mipango miji, mazingira na usafirishaji.

Mwita ambaye madiwani walimpigia kura ya kutokuwa na imani naye na kumng’oa, alifika katika ukumbi wa Karimjee leo Alhamisi Januari 23, 2020 na kukuta milango yote imefungwa, huku wajumbe wakiendelea na vikao.

Kabla ya kuingia katika viwanja vya Karimjee, askari waliokuwa getini walimzuia Mwita kwa maelezo kuwa wamepewa maelekezo.

Baada ya mvutano uliodumu kwa takribani nusu saa, Mwita aliingia katika viwanja vya ukumbi huo  lakini alikuta milango imefungwa.

Akizungumza kuhusu tukio hilo diwani wa Tabata, Patrick Assenga amesema yeye ni mwenyekiti wa kamati ya mipango miji, mazingira na usafirishaji na ndio alitakiwa kuongoza kikao.

"Kikao kilichotangulia ni cha huduma za jamii na kinachofuata ni cha mipango miji mazingira na usafirishaji, mimi ndio mwenyekiti wa kamati hiyo,” amesema Assenga.

Diwani huyo amesema Rais John Magufuli anatakiwa kuingilia sakata la Mwita kuondolewa kwa madai kuwa ni kinyume na taratibu huku akiwataja watu kadhaa kuhusika na mpango huo.

Kwa upande wake Mwita amesema mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Sporah Liana ndio msingi wa kinachotokea sasa.

“Wameshindwa kuniondoa kwa kura, wameninyang’anya  gari sasa wameamua kufunga milango nisiingie kwenye vikao vya kamati ambavyo kwa mujibu wa katiba mimi ni mjumbe" amesema Mwita

Amesema tangu alipochaguliwa kuwa Meya amekuwa akishiriki shughuli zote za Serikali.

"Nitaendelea kuwa meya hadi baraza litakapovunjwa,  asiyenitaka atafute kazi ya kufanya kura za kuniondoa hazikutosha wajumbe hawakufika mbili ya tatu,” amesema Mwita.

Liana alipopigiwa simu kuulizwa kuhusu suala hilo alijibu kuwa yupo kikaoni.

Kwa mujibu wa kanuni za kudumu za Halmashauri ya Jiji kifungu cha 84 (1) kinaeleza ili uamuzi uweze kufanyika wa kumwondoa meya madarakani kutokana na sababu kadhaa, itapaswa kuwapo kwa theluthi mbili ya wajumbe wa halmashauri hiyo.

Theluthi mbili ya wajumbe 26 wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ni 17. Kifungu hicho kinasomeka:

“Halmashauri inaweza kumuondoa meya madarakani kwa kupata azimio linaloungwa mkono na theluthi mbili ya wajumbe wa halmashauri kutokana na hoja au sababu yoyote zifuatazo mojawapo ni kutumia vibaya ofisi yake.”

Kikao maalumu cha baraza la madiwani la jiji hilo, Alhamisi iliyopita kilikutana kwa ajenda moja ya kupokea ripoti ya tuhuma dhidi ya Meya Mwita kisha kupiga kura ya kutokuwa na imani naye huku kura zilizomkataa zikiwa 16 pungufu ya matakwa ya kanuni za Halmashauri zinavyoelezwa.