Mwitikio mdogo vijana kupima VVU

Wananchi waliojitokeza kwenye uwanja wa shule ya sekondari Morogoro kwa ajili ya maadhimisho ya kitaifa ya siku ya Ukimwi duniani. Lilian Lucas

Muktasari:

  • Mtandao wa wanawake wakishirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo, wamejitosa kutoa elimu itakayosaidia kutokomeza maambukizi ya VVU kwa watoto wachanga, wasichana na wanawake.

Morogoro. Kasi ndogo ya upatikanaji elimu juu ya upimaji virusi vya Ukimwi kwa vijana, inatajwa kuwa sababu ya mwitikio mdogo wa vijana kujua afya zao,  hivyo kuhatarika juhudi za nchi kutokomeza maradhi hayo ifikapo 2030.

Hayo yamebainishwa leo Desemba Mosi, 2023  mjini Morogoro na Veronica Lyimo, ambaye ni Mkurugenzi wa Mtandao wa Kitaifa wa Wanawake Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (NNW+), alipofanya mahojiano maalumu na Mwananchi Digital.

“Kijana anatakiwa kuwa na uelewa juu ya mabadiliko ya mwili ili kumuweka salama na kuepuka kupata maambukizi ya VVU akiwa katika umri mdogo, ikiwa ni pamoja na kuepuka kushiriki ngono na kupata magonjwa mengine ambukizi,” amesema.

Aidha amesema kama wanawake katika kuleta sauti ya pamoja ya kutokomeza maambukizi ya ugonjwa huo  wamekuwa wakishirikiana na wadau wa maendeleo, kutoa elimu ili kutokomeza  maambukizi hayo kwa watoto wachanga, wasichana, na wanawake.

"Kama tunavyofahamu watoto wachanga, wanawake na mabinti, takwimu za maambukizi zinaonyesha yako juu kwa kundi hilo, sasa katika kushirikiana na wadau tunatarajia kuwa na jamii iliyo salama ifikapo 2030," amesema Lyimo.

Kwa mujibu wa Lyimo, programu mbalimbali za kutokomeza ukatili wa kijinsia na majumbani, pamoja na suala la afya ya uzazi kwa vijana hasa rika barehe mtandao wake umekuwa ukiziendesha.

"Hafua zipo za kutosha lakini changamoto ya hofu ya vijana kujua afya zao kwa kufikiria kuwa akijua atakatisha masomo na kadhalika, ni kundi ambalo linatakiwa kwenda nalo kwa hekima tofauti na mengine," amesema.

Hata hivyo amesema kuwa wanawake wamekuwa mstari wa mbele kujitokeza kupima VVU kuliko wanaume,  hiyo inatokana na wanaume kuwa na majukumu mengi, huku akieleza kama mtandao hawatachoka kufanya uhamasishaji.

Kwa upande wa Mratibu wa huduma za vijana kutoka Wizara ya Afya kwenye kitengo cha mpango wa kuthibiti Ukimwi, magonjwa ya ngono na homa ya ini, Patricia Kuya amesema mkakati wa wizara hiyo ni kuhakikisha maambukizi ya Ukimwi yanapungua kwa asilimia 95 ifikapo 2030.

Kuya amesema wizara imeweka mkakati wa kuanzisha mafunzo ya malezi kwa wazazi na vijana, hasa baada ya kuona kuwa kuna pengo katika jamii kutokana na wazazi kutozungumza na vijana wao kuhusu masuala ya afya ya uzazi hususani Ukimwi, mimba za utotoni na magonjwa ya ngono.

"Tunatoa elimu mbalimbali ikiwemo ya jipime, kwa vijana walio na umri wa kuanzia miaka 18, homa ya ini kwa vijana, na hiyo imetokana na maambukizi ya Ukimwi yapo juu  kwenye kundi la vijana hasa wa kike wenye umri kati miaka 15 hadi 24," amesema na kuongeza;

"Asilimia mbili ya vijana wa kike wameathirika na VVU na huo ni utafiti uliofanyika 2016 hadi 2017 ukilinganisha na vijana wa kiume, kwa hiyo mikakati mbalimbali imeendelea kufanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau kwenye masuala ya Ukimwi.”

Aidha, amesema kumekuwa na tatizo la vijana kutofuata matumizi ya dawa kwa usahihi, akihimiza  wazazi na walezi kuwasimamia ili kufubaza makali ya VVU.