Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwongozo wa taaluma mapema watajwa kuwa suluhisho kwa wanafunzi

Wanafunzi wa Shule ya Kimataifa ya Morogoro wakiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU) walipotembelea chuo hicho, jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujifunza masuala mbalimbali. 

Muktasari:

  • Wamesema wanafunzi wengi hufika kidato cha sita bila kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu uhusiano kati ya masomo wanayochagua na taaluma wanazoweza kuzifuata, hali inayowafanya kujiunga na kozi wasizozifahamu vizuri au kubadilisha mwelekeo wa masomo wakiwa wamefika elimu ya juu.

Dar es Salaam. Wadau wa elimu wameeleza kuwa ukosefu wa mwongozo wa taaluma kwa wanafunzi katika hatua za awali za elimu unachangia wengi kufanya uamuzi usiyo sahihi kuhusu masomo na taaluma zao za baadaye.

Wamesema wanafunzi wengi hufika kidato cha sita bila kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu uhusiano kati ya masomo wanayochagua na taaluma wanazoweza kuzifuata, hali inayowafanya kujiunga na kozi wasizozifahamu vizuri au kubadilisha mwelekeo wa masomo wakiwa tayari wamefika elimu ya juu.

Akizungumza wakati wa ziara ya wanafunzi wa Shule ya Kimataifa ya Morogoro katika Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU) jijini Dar es Salaam jana Ijumaa leo Juni 19, 2026, Ofisa wa Uandikishaji wa chuo hicho, Peter Mangi amesema mwongozo wa taaluma nchini mara nyingi huanza kuchelewa.

“Mara nyingi mwanafunzi huanza kufikiria taaluma yake akiwa kidato cha sita, wakati tayari ameshafanya uamuzi muhimu wa kielimu.

“Tunaamini ni muhimu kuwafikia wanafunzi mapema kuanzia Kidato cha Kwanza hadi cha Nne ili kupanga safari yao ya taaluma kwa uelewa zaidi,” amesema.


Mangi amesema AKU imekuwa ikitoa fursa kwa wanafunzi kutembelea chuo hicho ili kujifunza kuhusu taaluma mbalimbali, hususan katika sekta za afya, uuguzi na sayansi.

Kwa mujibu wa Mangi, wanafunzi wanapaswa kuanza kujifunza kuhusu fursa za elimu ya juu mapema zaidi ili waweze kufanya maamuzi sahihi ya kitaaluma kabla ya kuchagua mchepuo wa masomo.

“Chuo kinaamini ni muhimu kuwafahamisha wanafunzi kuhusu elimu bora ya juu tangu hatua za awali, kuanzia kidato cha kwanza hadi kidato cha nne,” ameeleza.

Changamoto hiyo si ya Tanzania pekee. Tafiti mbalimbali barani Afrika zimeonyesha kuwa ukosefu wa mwongozo wa taaluma huchangia wanafunzi kuchagua kozi zisizowafaa, kupungua kwa hamasa ya kujifunza na hata kuongezeka kwa kiwango cha wanaoacha masomo katika elimu ya juu.

Mwanafunzi wa Shule ya Kimataifa ya Morogoro, Myra Mbotto-Malugu (15), amesema ziara hiyo imemsaidia kuelewa vyema njia za kielimu zinazohitajika kufikia taaluma anazozifikiria.

“Nimekuwa nikifikiria kati ya urubani na sayansi za afya. Kupitia semina hii nimepata mwanga kuhusu masomo ninayopaswa kusoma na hatua za kufuata ili kufikia malengo yangu,” amesema.

Mwalimu wa shule hiyo, Azizi Amimungalawa, amesema taasisi hiyo huandaa ziara za kielimu kwa makusudi ili kuwasaidia wanafunzi kuhusisha wanachojifunza darasani na mazingira halisi ya kazi.

“Tunataka wanafunzi wafahamu mapema fursa zilizopo katika ulimwengu wa ajira. Wanapokutana na wataalamu na wanafunzi wa vyuo vikuu, hupata picha halisi ya taaluma wanazoweza kuzifuata na maandalizi yanayohitajika,” amesema.

Amesema ziara za kielimu, programu za ushauri na ulezi (mentorship), pamoja na mazungumzo na wataalamu wa sekta mbalimbali, ni miongoni mwa njia muhimu zinazowasaidia wanafunzi kufanya uamuzi sahihi ya taaluma na kujiandaa kwa mahitaji ya soko la ajira la baadaye.

Katika ziara hiyo, wanafunzi walishiriki mijadala ya taaluma, walikutana na wanafunzi wa AKU na kutembelea vituo vya kujifunzia, ikiwemo vituo vya ubunifu na maabara za mafunzo ya vitendo vinavyowaonesha mazingira halisi ya huduma za afya.