Mzazi amkamata kijana akimtuhumu kumrubuni binti yake

Muktasari:

  • Mzazi huyo alimkamata kijana huyo na kumfikisha shuleni kwa binti yake walipokuwepo wataalamu wa sheria waliokuwa wakitoa elimu ya sheria ikiwa mwendelezo wa wiki ya sheria na kumlalamikia.

Kiteto. Alais Salasaita ambaye ni mzazi wa mwanafunzi wa kidato cha pili shule ya sekondari ya Kibaya mkoani Manyara (jina limehifadhiwa), amemkamata Nasibu Heri (18), akimtuhumu kumpa simu ya mkononi kwa lengo la kumtaka kimapenzi.

Mzazi huyo amedai kuwa mwenendo wa binti yake umekuwa mbaya ikiwa pamoja na kuwa mtoro shuleni.
Tukio hili limetokea Januari 24, 2023 baada Alais Salasaita kumkamata Heri na kumfikisha katika shule hiyo, ambako walikuta jopo la wanasheria, waendesha mashataka, mkuu wa Dawati la Jinsia la Polisi waliokuwa wakitoa elimu ya sheria ikiwa mwendelezo wa wiki ya sheria.
"Jana na juzi tumewasikia mkitutaka kuwa makini kufuatilia watoto wetu sasa mimi nimemkamata mwenyewe mhalifu wangu naomba mnisaidie sheria ifuate mkondo wake huyu ameamua kuharibu maisha ya mwanangu," amesema Salasaita.
Baada ya kusikia malalamiko ya mzazi huyo, Mkuu wa shule hiyo, Cornel Mchomvu amekiri kuwepo kwa vitendo vya ukatili hapo shuleni akisema mara kadhaa amekuwa akiviripoti mamlaka husika.
"Bahati nzuri leo timu imekamilika hapa Mkuu wa Dawati la Polisi yupo, Mwendesha mashtaka wa Serikali yupo, hakimu na wadau wengine wa sheria mpo naomba tuanzie na huyu kisha wengine watafuata,” amesema.
Akishauri namna bora ya kushughilikia tukio hili, Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Kiteto, Mosi Sassy ameshauri mtuhumiwa huyo kufikishwa Polisi kwa hatua zaidi
"Ni vizuri mtuhumiwa huyu akafikishwa Polisi kwa upelelezi kisha wakiona kuna kesi ya kujibu atafikishwa mamlaka husika kwa hatua zaidi," amesema.