Mzigo unaomsubiri Mwandosya Ewura
Muktasari:
- Waziri wa zamani, Profesa Mark Mwandosya anakabiliwa na jukumu kubwa la kudhibiti ongezeko la bei ya mafuta baada ya kuteuliwa kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura).
Dar es Salaam. Waziri wa zamani, Profesa Mark Mwandosya anakabiliwa na jukumu kubwa la kudhibiti ongezeko la bei ya mafuta baada ya kuteuliwa kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura).
Juzi, Rais Samia Suluhu Hassan alimteua Profesa Mwandosya kuwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa Ewura, akichukua nafasi ya Profesa Jamidu Hazzam, ambaye amemaliza muda wake.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais - Ikulu, Zuhura Yunus, uteuzi wa Profesa Mwandosya umeanza Agosti 15, mwaka huu.
Akizungumza na Mwananchi kuhusu uteuzi huo, Profesa Mwandosya alisema atakwenda kushirikiana na wakurugenzi wenzake wa bodi kuhakikisha wanakidhi matarajio ya Rais na wananchi kwa ujumla.
“Kwa unyenyekevu mkubwa natoa shukrani kwa aliyeniteua (Rais Samia) na kwamba, mimi ni mmoja tu kati ya wakurugenzi ambao ni wajumbe wa bodi, kwa hiyo tutafanya kazi kukidhi matarajio ya mamlaka ya uteuzi na wananchi,” alisema Profesa Mwandosya.
Profesa Mwandosya ni mwanasiasa mkongwe aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, ikiwa ni pamoja na uwaziri katika wizara mbalimbali, mkurugenzi wa mashirika ya umma, mwenyekiti wa bodi za taasisi mbalimbali na mbunge.
Amekuwa nje ya ulingo wa siasa kwa miaka saba na katika kipindi hicho amekuwa akitumia mtandao wa kijamii Twitter kutoa maoni yake. Amekuwa mkosoaji mkubwa wa baadhi ya mambo ambayo anaona hayaendi sawa na kuibua mijadala.
Profesa Mwandosya, aliyezaliwa mwaka 1949, aliwahi kuwa mbunge wa Rungwe Mashariki kupitia CCM kuanzia Novemba 2000 hadi Julai mwaka 2015 alipoamua kustaafu.
Licha ya kuwa mbunge, aliwahi kuwa Waziri katika Ofisi ya Rais (2013 – 2015), Wizara ya Maji (2010 – 2013), Wizara ya Maji na Umwagiliaji (2008 – 2010), Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira (2006 – 2007) na Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi (2000 – 2005).
Pia amewahi kuwa Katibu Mkuu katika Wizara za Viwanda na Biashara (1993 – 1994), Maji, Nishati na Madini (1990 – 1992) pamoja na Kamishna wa Tume ya Nishati na Mambo ya Petroli (1985 – 1990).
Profesa Mwandosya, ambaye kitaaluma ni mhandisi wa umeme, anakwenda kusimamia Ewura ambayo imepewa mamlaka ya kusimamia bei za huduma na kufuatilia maendeleo ya sekta zinazodhibitiwa kwa kuzingatia upatikanaji, ubora wa huduma, gharama ya huduma, ufanisi wa uzalishaji, uwekezaji na usambazaji wa huduma.
Tangu mlipuko wa janga la Uviko-19 ulipotokea duniani mwishoni mwa mwaka 2019 pamoja na vita kati ya Ukraine na Russia, bei za mafuta zimezidi kupanda katika soko la dunia, jambo ambalo limesababisha kupaa kwa bei ya bidhaa hiyo hapa nchini.
Wananchi wamekuwa wakilia gharama kubwa za mafuta ambazo zimesababisha pia kupaa kwa bei za bidhaa na huduma mbalimbali pamoja na kusababisha ugumu wa maisha kwa wananchi wa kawaida.
Kutokana na hali hiyo, Serikali iliamua kutoa ruzuku ya mafuta ya Sh100 bilioni kila mwezi, ili kushusha bei na kuleta unafuu kwa wananchi. Hata hivyo, inaelezwa kwamba bila ruzuku hiyo, bei ya mafuta ingekuwa juu zaidi.
Agosti 2, Ewura ilitangaza bei mpya za mafuta ambapo bei ya rejareja Dar es Salaam ni Sh3,410 kwa lita moja ya petroli na Sh3,322 kwa dizeli, huku mafuta ya taa yakifika Sh3,765.
Viwango hivyo vinaonyesha bei imepanda zaidi mwezi huu na kuivuka ile ya Julai 2022 ambapo petroli imepanda kwa Sh190 kwa kila lita na Sh179 kwa kila lita ya dizeli, huku mafuta ya taa yakipanda kwa Sh323 kwa kila lita kwa Jiji la Dar es Salaam.
Jukumu jingine la Ewura ni usimamizi wa gharama za huduma za maji zinazosimamiwa na mamlaka mbalimbali za maji, ambazo zimekuwa zikipanga bei kulingana maeneo husika na wakati mwingine kuibua mvutano baina yao na wananchi.
Aidha, mwanasiasa huyo atakuwa na jukumu jingine la kusimamia bei za gesi ambazo nazo zimekuwa zikipanda na kuibua sintofahamu kwa wananchi.
Katika ukurasa rasmi wa Ikulu wa Twitter walipoweka taarifa ya uteuzi wake, baadhi ya wananchi walichangia wakisema;
@EnziNaEnzi alisema, “hongera yake! Katupunguzie bei za gasi ya kupikia na gharama za kuvuta umeme, kwenye maji hapo kamanda Aweso (Jumaa Aweso-Waziri wa Maji) anaupiga mwingi mnooo.”
Naye @pius_mponzi alisema, “hongera Prof. Mwandosya kwa uteuzi huu, ni matumaini yangu kuwa utautumia uzoefu wako katika sekta ndogo ya nishati ipasavyo na kuyatekeleza kwa vitendo yaliyomo kwenye machapisho yako ya kitaaluma.”
…ni mtu sahihi
Mtaalamu wa uchumi, Dk Abel Kinyondo alisema Profesa Mwandosya anakabiliwa na jukumu la kupunguza utegemezi wa mafuta kama chanzo cha nishati badala yake kugeukia vyanzo vingine kama sola na gesi.
“Profesa anachukua nafasi hii katika kipindi ambacho dunia inahama kutoka kwenye vyanzo vya nishati chafu kama petroli, dizeli, mafuta ya taa kwenda kwenye nishati safi kwa maana ya nishati ya nguvu za jua na upepo.
“Kwa hiyo ameingia kwenye changamoto kwamba Tanzania tunahama, tunahama lini, tunahamaje katika kipindi ambacho kwa umasikini wa wananchi wetu, kuna ambao hata hawajahama kutoka kwenye kuni kwenda kwenye mkaa, lakini dunia inasema si tu mkaa, hatutaki hata mafuta ya petroli,” alisema.
Dk Kinyondo alisema si tu anakabiliwa na changamoto ya kushusha bei ya nishati isiendelee kupanda, bali pia kuhama kutoka kwenye utegemezi wa mafuta ya kisukuku (fossil fuel) kwenda katika nishati ambazo ni safi.
Kwa upande wake, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Profesa Humphrey Moshi alisema uteuzi wa Profesa Mwandosya ni mzuri kwa sababu ana uzoefu na alishiriki katika kuandika Dira ya Taifa ya 2025.
“Mwandosya ameshirikiana na wachumi waliobobea katika uchumi…tulikuwa naye katika kuandaa Dira ya Taifa ya 2025, kwa hiyo huu uzoefu anao, halafu jina lake ni kubwa, haliko tu Tanzania, liko duniani, kwa hiyo huo ni uteuzi mzuri,” alisema.
Profesa Moshi alisema kosa kubwa lililofanyika nchini ni kuweka tozo nyingi kwenye mafuta kwa sababu ni bidhaa ambayo ikipanda bei, bidhaa nyingine zote zitapanda bei na kuathiri wananchi wote.