Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NaCoNGO, LSF zaingia makubaliano kuimarisha uwezo wa mashirika ya kiraia

Katibu Mkuu wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Fransisca Mboya (kushoto), akiwa na Meneja Mipango wa LSF, George Mollel (kulia), wakifurahia jambo baada ya kutia saini makubaliano ya kushirikiana.

Muktasari:

  • Makubaliano ya NaCoNGO na LSF yanatarajiwa kuimarisha sekta ya mashirika yasiyo ya kiserikali nchini na kuongeza mchango wake katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Dar es Salaam. Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) kwa kushirikiana na Shirika la Huduma za Kisheria (LSF) zimesaini hati ya makubaliano (MoU) yenye lengo la kuimarisha uwezo wa mashirika ya kiraia nchini, hususan katika uongozi, utafutaji wa rasilimali na kuboresha utoaji wa huduma kwa jamii.

Makubaliano hayo yamesainiwa Juni 11, 2026 jijini Dar es Salaam, yakilenga pia kuweka mazingira wezeshi ya utendaji kazi wa mashirika hayo pamoja na kuimarisha ushirikiano wake na Serikali.

Akizungumza baada ya hafla ya utiaji saini, Katibu Mkuu wa NaCoNGO, Fransisca Mboya, amesema ushirikiano huo utaongeza ufanisi wa mashirika yasiyo ya kiserikali na kupunguza changamoto zinazokwamisha utekelezaji wa majukumu yake.

Amesema maeneo makuu yatakayopatiwa kipaumbele ni kujengea uwezo viongozi katika utafutaji wa rasilimali, kuboresha mazingira ya kazi kwa mashirika hayo na kuimarisha ushirikiano na Serikali.

“Tumekuwa tukishirikiana kwa muda mrefu, lakini sasa tumeweka rasmi makubaliano haya ili kuongeza ufanisi na matokeo chanya katika kazi zetu,” amesema Mboya.

Kwa upande wake, mwakilishi wa LSF, George Mollel, amesema makubaliano hayo ni hatua ya kuimarisha ushirikiano uliokuwepo na kuongeza wigo wa kufikia jamii kwa ufanisi zaidi.

Amesema LSF inatambua nafasi ya NaCoNGO katika kuratibu mashirika ya kiraia nchini na mchango wake katika maendeleo ya kijamii.

“Lengo ni kuhakikisha mashirika yasiyo ya kiserikali yanafanya kazi bila vikwazo vinavyoweza kuathiri utendaji wao,” amesema Mollel.

Ameongeza kuwa kupitia ushirikiano huo, mashirika yatapatiwa mafunzo na msaada wa kitaalamu utakaowawezesha kuboresha ubunifu na kuongeza uwezo wa kujitegemea kifedha.

Makubaliano hayo yanatarajiwa kuimarisha sekta ya mashirika yasiyo ya kiserikali nchini na kuongeza mchango wake katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.