Naibu Waziri awataka wachimbaji kuacha utoroshaji dhahabu

Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa akipata maelekezo kutoka kwa Afisa Masoko na Mauzo wa kampuni ya GF Trucks & Equipment’s Ltd Smart  Peter  William wakati alipotembelea banda lao kwenye maonyesho ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea Chunya mkoani Mbeya.

Chunya. Naibu Waziri wa Madini, Steveni Kiruswa amewataka wachimbaji wa madini kuachana na utoroshaji wa madini dhahabu na kutumia masoko yaliopo kufuatia masoko hayo kuonyesha mchango mkubwa serikalini.

Kiruswa ametoa kauli hiyo wakati akizungumza katika uzinduzi wa Maonyesho ya teknolojia ya madini na uwekezaji Mkoa wa Mbeya ambayo yanafanyika Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya.

Amesema tangu kuanzishwa kwa masoko ya madini nchini sekta hiyo imekuwa ikimalika siku hadi siku ambapo toka mwaka 2017 mchango wake ilikuwa likichangia asilimia 4.4 na kwa sasa imefikia asilimia  9.7.

Pia, aliwataka wachimbaji kutumia maonyesho hayo kwa kujifunza kwani makampuni mbalimbali yameshiriki maonyesho hayo watapata namna bora ya kubadilishana uzoefu katika kwenye uwekeza wa madini.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera akizungumza katika maonyesho hayo amesema lengo la kuandaa maonyesho kimkoa ni kutaka wachimbaji wa madini wajifunze namna bora ya kuzalisha madini na kukuwajengea uwezo wa kuongeza thamani ya madini.

Homera amesema uwepo wa masoko na mazingira bora  kwa wachimbaji wa madini ya dhahabu umesababisha leseni za uchenjuaji wa madini kuongezeka kutoka leseni 4 mpaka 250. Leseni za wafanyabiashara wa madini zimeongezeka kutoka leseni 0 mpaka 300 na wafanyabiashara wakubwa kutoka 0 mpaka 60 hali aliyodai kuwa imeongeza uzalishaji wa madini kutoka kilo 250 kwa mwezi mpaka kilo 300.

Aidha, Sabai Nyasiri ambaye ni Ofisa Madini mkazi Mkoa wa Kimadini Chunya, amesema maonesho hayo ya teknolojia ya madini yatakwenda sambamba na kongamano la madini litalohusisha wadau mbalimbali ili kujadili changamoto zinazowakabili wachimbaji wa dhahabu na namna bora ya kuzitatua.

Naye mmoja wa wauzaji wa vifaa vya migodini, Afisa Masoko na Mawasiliano wa Kampuni ya GF Trucks & Equipments Ltd, Smart Deus amesema kampuni hiyo imejikita kuwasaidia wachimbaji wadogo wadogo na hivyo inamapango maalumu wa kuhakikisha inawapatia mikopo ya mashine za kuchimbia kwa mashariti nafuu kwa kushirikiana na benki rafiki ambazo zimeingia makubaliano ya kuwakopesha vifaa na siyo pesa ili kuwainua wachimbaji wadogo.

Hata hivyo, mmoja wa wanunuzi wa dhahabu waliohudhuria maonyesho ya uwekezaji Deus Lugatius amesema kwa Wilaya ya Chunya kuletewa maonesho hayo ni fursa ya teknolojia ya madini na uwekezaji ni fursa kwao kujifunza teknolojia mpya ili waweze kubora kazi zao.