Naibu Waziri Nderiananga aonya wanaoficha watu wenye ulemavu wakati wa sensa

Naibu Waziri Nderiananga aonya wanaoficha watu wenye ulemavu wakati wa sensa

Muktasari:

  • Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye ulemavu, Ummy Nderiananga ameitaka jamii, kuacha kuwaficha ndani watu wenye ulemavu na kuhakikisha wakati wa sensa ya watu na makazi mwakani.

  

Moshi. Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye ulemavu, Ummy Nderiananga ameitaka jamii, kuacha kuwaficha ndani watu wenye ulemavu na kuhakikisha wakati wa sensa ya watu na makazi mwakani.

Waziri Ummy ametoa rai hiyo leo Oktoba 20, 2021 wakati akizungumza kwenye semina ya madiwani wanawake Mkoa wa Kilimanjaro, inayofanyika mjini Moshi, ambapo amesema kupatikana kwa takwimu sahihi za kundi hilo kutaiwezesha serikali kupeleka huduma nzuri zaidi.

"Mwakani tuna sensa ya watu na makazi, niwaombe madiwani kuhamasisha jamii kushiriki kuhesabiwa na kwenye kundi la watu wenye ulemavu tuweke mkazo wasije wakafichwa ndani bali tupate takwimu zao sahihi ili tunapopanga mipango ya maendeleo tujue wako wangapi," amesema Ummy.

Aidha, ameitaka pia jamii kuendelea kuwapenda na kuwathamini watu wenye ulemavu na kuhakikisha wanapata haki zao za kimsingi kama ilivyo kwa watu wasio na ulemavu.

Akizungumza mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi amewataka Madiwani hao kutoa elimu kwa jamii kueleza umuhimu wa kuhesabiwa katika maeneo yao, ili kuhakikisha zoezi la Sensa linapoanza wote wanakuwa na uelewa.


"Kumekuwepo na baadhi ya watu, ambao wana mtazamo potofu kuhusu kuhesabiwa, niwaombe madiwani, mko kule kwenye jamii, waelimisheni wananchi wote wanakuwa na uelewa, na wakati utakapofika wote wahesabiwe, ili iwe rahisi kwa serikali kuleta maendeleo," amesema.

Mafunzo hayo ambayo yaliandaliwa na Naibu waziri huyo, na kutolewa na wataalamu kutoka Wizara ya Sheria na Katiba, ililenga kuwajengea uwezo madiwani hao na kuwawezesha kufahamu, haki, sheria, wajibu na miongozo wanayopaswa kusimamia kama madiwani wanawake.