Naibu waziri utalii aongoza wanawake Hifadhi ya Tarangire

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja akizungumza na Wanawake kutoka taasisi za serikali na binafsi kabla ya kutembelea Hifadhi ya Taifa Tarangire kuadhimisha Siku ya Wanawake duniani leo.Picha na Filbert Rweyemamu

Muktasari:

  • Naibu  Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja ameongoza wanawake kusherekea siku ya wanawake duniani kwa kutembelea Hifadhi ya Taifa Tarangire.

 Arusha. Naibu  Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja ameongoza wanawake kusherekea siku ya wanawake duniani kwa kutembelea Hifadhi ya Taifa Tarangire.

Akizungumza na watalii hao wa ndani kutoka taasisi za Serikali na binafsi mkoani Arusha, amesema wanawake wameonyesha uwezo mkubwa katika uongozi akitoa mfano wa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.

"Wanawake tunaweza kutoa mchango mkubwa wa maendeleo ya nchi yetu kwa kuhakikisha tunashiriki kikamilifu ujenzi wa Taifa letu katika nyanja mbalimbali zikiwemo kuwekeza kwenye sekta ya utalii," amesema.

Meneja mawasiliano kwa umma wa Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro (NCAA), Joyce Mgaya amesema hatua ya Masanja kuungana na wanawake  kutalii pamoja kunawapa faraja wanawake wote kusherekea siku yao.

“Nimefurahishwa sana na kitendo cha kiongozi wetu Masanja kutambua na kuthamini mchango wa wanawake wanaofanya kazi ndani ya wizara anayoisimamia. Tumekuwa na viongozi wengi lakini huyu ameonyesha mfano wa kipekee hatuna budi kumshukuru," amesema Joyce