Naibu Waziri wa Maliasili awapa ‘tano’ TAWA

Muktasari:

  • Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa kazi nzuri ya usimamizi wa rasilimali za wanyamapori nchini huku akisisitiza nidhamu na uadilifu kwa watumishi wote wa mamlaka hiyo.

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa kazi nzuri ya usimamizi wa rasilimali za wanyamapori nchini huku akisisitiza nidhamu na uadilifu kwa watumishi wote wa mamlaka hiyo.

Ametoa pongezi hizo, alipotembelea ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) zilizopo mkoani Morogoro na kuzungumza na menejimenti na watumishi wa mamlaka hiyo kuhusu masuala mbalimbali yanayoihusu mamlaka, ikiwa ni muendelezo wa ziara zake katika Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Masanja amesema "Pamoja na uchanga na uchache wenu kwenye Wizara mmeweza kushikamana vizuri, mmepokea majukumu yenu na mnafanya kazi nzuri usiku na mchana", amesema Masanja nakuongeza

"Tufanye kazi kwa uadilifu tukiziangalia kanuni zetu za Jeshi la Uhifadhi, wale wachache wanaopaka madoa Jeshi letu tuwaepuke na ikiwezekana tuwaripoti", amesisitiza.

Katika ziara hiyo Masanja ameiagiza TAWA kuongeza kasi ya utekelezaji wa mikakati ya kudhibiti wanyama wakali na waharibifu ikiwemo, zoezi endelevu la utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu namna bora ya kujilinda na wanyamapori wakali na kuongeza kasi ya ujenzi wa vituo vidogo vya kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu.

Awali, akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa TAWA, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi Mabula Misungwi Nyanda, amezungumzia masuala mbalimbali yakiwemo majukumu ya TAWA, mafanikio na changamoto mbalimbali zinazoikabili Mamlaka ikiwemo suala mtambuka linalohusu wanyamapori wakali na waharibifu.

Pia, Kamishna Mabula amemshukuru Masanja kwa kutenga muda wake kuitembelea TAWA na kuahidi kutekeleza maagizo yote aliyoyatoa.