Nani alimuua dada wa Bilionea Msuya? hukumu leo

Miriam Steven Mrita, mjane marehemu Erasto Msuya, maarufu kama Bilionea Msuya; akiwa na Wakili wake Peter Kibatala

Muktasari:

  • Katika kesi hiyo ya jinai namba 103 ya mwaka 2018, Miriam na mwenzake Muyella wanadaiwa kutenda kosa hilo la mauaji ya kukusudia Mei 26, 2016 huko nyumbani kwa Aneth Kibada, Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, leo inatarajiwa kutoa hukumu ya kesi ya mauaji inayomkabili Miriam Steven Mrita, mjane wa aliyekuwa mfanyabiashara maarufu wa madini mkoani Arusha, bilionea Erasto Msuya.

Miriam pamoja na mshitakiwa mwenzake, Revocatus Everist Muyella, maarufu kama Ray, wanakabiliwa na shitaka la mauaji ya kukusudia, wanadaiwa kumuua kwa kumchinja, Aneth Elisaria Msuya ambaye ni wifi yake Miriam.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 103 ya mwaka 2018, Miriam na mwenzake Muyella wanadaiwa kutenda kosa hilo la mauaji ya kukusudia Mei 26, 2016 huko nyumbani kwa Aneth Kibada, Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Aneth alikuwa mdogo wa Bilionea Msuya, aliyeuawa kwa kupigwa risasi kwa kutumia bunduki ya kivita aina ya SMG katika eneo la Mijohoroni, barabara kuu ya Moshi-Arusha wilayani Hai, Mkoa wa  Kilimanjaro, Agosti 7, 2013.

Hukumu hiyo inayotarajiwa kusomwa na Jaji Edwin Kakolaki aliyeisikiliza kesi hiyo, ndio itakayoamua hatima yao iwapo wana hatia au la na iwapo wana hatia, adhabu ni kunyongwa hadi kufa na kama hawana, wanaweza kuachiwa huru.

Mpaka leo hukumu hiyo inapotolewa, washtakiwa wameishi mahabusu kwa takribani miaka minane wakisubiri kukamilika kwa usikilizwaji wa kesi, kwa kuwa shtaka la mauaji linalowakabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria nchini.


Ramani ya hukumu

Katika kuamua kesi hiyo iwapo washtakiwa wana hatia au la, Mahakama itachambua ushahidi wa upande wa mashtaka na wa utetezi na kuupima katika mizania ya sheria kuona kama umekidhi vigezo na masharti ya kisheria.

Sheria hizo ni Katiba, sheria ya mwenendo wa makosa ya Jinai nchini (CPA), kesi rejea ambazo ni hukumu na maamuzi ya kesi mbalimbali zilizokwishaamriwa na Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufani katika hoja au masuala yanayofanana na kesi husika.

Kisheria,  upande wa mashtaka ndio una dhima ya kuthibitisha mashtaka ya jinai dhidi ya mshtakiwa kwa kiwango cha kutoacha mashaka yoyote,  na ni kanuni ya kisheria kuwa mshtakiwa hawezi kutiwa hatiani kwa sababu tu ya udhaifu wa utetezi wake, bali kutokana na uzito wa ushahidi wa upande wa mashtaka.

Hivyo upande wa utetezi au mshtakiwa hawajibiki kuthibitisha kutotenda kosa na wajibu wake ni kuibua tu mashaka dhidi ya ushahidi wa upande wa mashtaka, yatakayopunguza uzito wake na hivyo kuufanya kutoaminiwa na Mahakama.

Kwa hiyo mahakama ili kufikia hitimisho la kama washtakiwa hao wana hatia au la, itaangalia ushahidi kwa ujumla wake kama umeweza au haukuweza kujibu pamoja na maswali, kama washtakiwa ndio wanaohusika na mauaji hayo.

Ikiwa Mahakama itaona kuwa ushahidi umethibitisha kuwa ndio waliohusika, basi itaangalia pia kama walifanya kitendo hicho kwa nia ovu.

Hivyo ili mahakama iwatie hatiani kwa kosa la mauaji (ya kukusudia, kama wanavyoshtakiwa, ushahidi wa upande wa mashtaka, unapaswa uthibitishe kuwepo kwa nia ovu.

Nia ovu kwa mujibu kifungu cha 200 cha Sheria ya Kanuni ya adhabu, inathibitishwa pamoja na dhamira ya kutenda kitendo hicho na ufahamu wa madhara ya kitendo husika.

Aina na ushahidi wa upande wa mashtaka uliopo

Upande wa mashtaka umejenga kesi yake katika ushahidi wa kimazingira kwa kuwa hakuna ushahidi wa moja kwa moja kwa maana kwamba hakuna shahidi aliyeshuhudia washtakiwa hao wakitekeleza mauaji hayo.

Kati ya mashahidi 25 walioitwa mahakamani hapo kuthibitisha shtaka hilo, msingi wa ushahidi wa upande wa mashtaka umejengwa kwa shahidi mmoja.

Huyu ni shahidi wa 25, Getruda Peniel Mfuru, aliyekuwa mfanyakazi wa kazi za ndani wa marehemu na ushahidi wa mashahidi wengine inasaidia kuunga tu mkono ushahidi wa shahidi huyo.

Getruda katika ushahidi wake, pamoja na mambo mengine alieleza kuwa alikutana na washtakiwa mara tatu kwa siku tofauti yaani Mei 15, 18 na 23, 2016 walipokwenda Kigamboni kutafuta mahali alikokuwa anaishi Aneth na kufanya mipango ya utekelezaji wa mauaji hayo.

Alidai washtakiwa walimwambia kuwa kuna kazi wanataka kuifanya kwa mwajiri wake, huku wakiahidi kumpatia Sh50 milioni kama wataikamilisha na wakamtaka ikifika Mei 25, 2016 asiwepo nyumbani naye akatii ndipo kesho yake akasikia kuwa mwajiri wake huyo alikuwa amechinjwa.


Utetezi na hoja za washtakiwa

Hata hivyo, washtakiwa hao walikana mashtaka na maelezo ya mashahidi hao.

Katika utetezi wao pamoja na hoja za mwisho za mawakili wao, Peter Kibatala anayemtetea Miriam na Nehemia Nkoko anayemtetea Muyella akiibua hoja zinazokusudia kuutikisa ushahidi wa upande wa mashtaka kwa kuonesha mashaka yatakayoishawishi mahakama isiuthamini.

Miongoni mwa hoja hizo zinazokusudia kuibua mashaka dhidi ya ushahidi wa Jamhuri na ambazo zinaweza kuwanufaisha kama mahakama itashawishika nazo ni pamoja na nia ovu, mkanganyiko wa ushahidi na ubovu hati ya mashitaka.

Nia ovu ya kutenda kosa

Katika kesi za mauaji nia ovu ni kigezo muhimu sana katika kuthibitisha mashtaka.

Upande wa mashtaka walidai mshtakiwa wa kwanza (Miriam) alitenda kosa hilo kwa kuwa alikuwa na mgogoro wa mali (mirathi ya marehemu mumewe, Bilionea Msuya) na marehemu Aneth na kwamba mshtakiwa na Aneth walikuwa wakitumiana ujumbe wa  kutukanana kwenye simu.

Lakini Wakili Kibatala alidai kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mgogoro huo kwani hakuna hata ndugu mmoja aliyekuja kuthibitisha kuwa mshtakiwa alikuwa na mgogoro wa aina yoyote ile na mshtakiwa wa kwanza.

Wakati akijtetea Miriam pia aliieleza mahakama kuwa licha ya kwamba simu zake na za marehemu zilichukuliwa na polisi, lakini hawakuwasilisha ushahidi wa ujumbe huo mahakamani kuthibitisha kuwepo ugomvi baina yake na Aneth.


Mkanganyiko wa mashahidi

Wakili Kibatala alidai kuwa shaidi wa kwanza wa Jamhuri, WP Mwajuma na shahidi wa 10 , Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) Richard Mchomvu walitofautiana kuhusu maelezo ya mshtakiwa.

Wakati WP Mwajuma akidai alielekezwa na ACP Mchomvu aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi mkoa wa Temeke (RCO) wakati huo, kuandika maelezo ya Miriam ambayo anakiri kutenda kosa, ACP Mchomvu alikana kuwa hakuwahi kumwelekeza WP Mwaka kuandika maelezo ya mshtakiwa huyo.

Pia alidai kuwa mashahidi wengine wawili ambao ni maafisa wa Polisi walipingana pamoja na kuwasilisha vielelezo viwili vinavyopingana kuhusu kukamatwa na kuhojiwa kwa mfanyakazi huyo wa ndani wa marehemu.

Shahidi mmoja anadai kuwa binti huyo alikamatwa na kuhojiwa kama mtuhumiwa lakini shahidi mwingine anadai kuwa binti huyo hakuwahi kukamatwa na kuhojiwa.

Hata hivyo tofauti hizo za mashahidi zinaweza kuwanufaisha washtakiwa ikiwa mahakama itaona kuwa zinaathiri hoja za msingi.


Ubovu wa hati ya mashtaka

Wakili Nkonko alidai kuwa hati ya mashtaka ina kasoro kwani inapingana na ushahidi uliowasilishwa mahakamani kwani tarehe, muda na eneo lilikotokea tukio vinatofautiana baina ya hati ya mashtaka na ushahidi uliowasilishwa.

Alidai kuwa majina ya mshtakiwa wa pili kwenye hati ya mashtaka ni tofauti na majina yake halisi. Mshtakiwa alishayakana tangu wakati wa usikilizwaji wa awali, lakini upande wa mashtaka haukuchukua hatua kufanya marekebisho ya hati ya maashtaka kwa mujibu wa sheria.

Aliielekeza Mahakama katika uamuzi wa kesi mbalimbali ilishaweka msimamoo kuwa katika mazingira hayo, Mahakama inapaswa kuifuta hati hiyo na kuwaachia huru washtakiwa.


Kanuni ya mtu wa mwisho kuonekana na marehemu

Katika kesi za ushahidi wa mazingira mtu wa kwanza kuhisiwa kuwa muuaji ni yule wa mwisho kuonekana na marehemu.

Mawakili wote kwa nyakati tofauti walieleza mahakama kuwa kwa ushahidi ulioko mahakamani, mtu wa mwisho kuwa na Aneth kabla ya kifo chake ni shahidi wa 25 wa upande wa mashtaka yaani  mfanyakazi wake wa kazi za ndani.

Hivyo waliiomba mahakama imuone kuwa shahidi huyo kuwa ndiye anayehusika na mauaji ya mwajiri wake huyo.