Nape aiita sekta binafsi ulinzi anga mtandao

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye akizungumza na wadau wa sekta hiyo mkoani Arusha. Picha na Bertha Ismail

Muktasari:

Serikali imewataka wadau wa sekta binafsi kushirikiana na sekta ya umma kuimarisha ulinzi na usalama katika anga ya mtandao.

Arusha. Serikali imewataka wadau wa sekta binafsi kushirikiana na sekta ya umma kuimarisha ulinzi na usalama katika anga ya mtandao.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu Machi 18, 2024 jijini Arusha na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye kwenye kikao cha tathimini ya sekta hiyo na wadau wake.

Amesema anga la mtandao likiwa salama ni faida kwa sekta binafsi kibiashara,  lakini pia nchi itakuwa salama na Watanzania watakuwa na imani ya kutumia mtandao kibiashara.

“Hivyo nizielekeze taasisi za umma kuweka misingi mizuri ya kisheria na kuisimamia, lakini kuondoa vikwazo visivyo na tija hasa katika uwekezaji wa miundombinu hii ili kuhakikisha usalama wa anga wa kimtandao unafanikiwa,” amesema Nape.

Mbali na hilo, Nnauye amesema wizara yake inaendelea kutekeleza wito wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kuvibeba vyombo vya habari kwa tija na maendeleo ya Taifa.

Amesema kupitia wito huo, yako mabadiliko makubwa yaliyofanyika katika usimamizi wa vyombo vya habari ikiwemo kuepuka kuchapana viboko vya faini na kufungiana.

“Sekta ya utangazaji zamani mkiandikiwa barua mnaandaa faini kabla ya kwenda, leo mkiona barua mnakimbia na mnaenda kupewa kahawa na juisi na kushauriwa. Habari Maelezo sijasikia kesi siku nyingi wala kusikia gazeti limefungiwa, hayo ni mageuzi makubwa yamefanyika kwenye namna tunavyoshughulika na sekta yetu,” amesema Nape.

Amesema sio kwamba kwa sasa makosa hayapo, bali wanatumia busara hata panapotokea  kasoro ndogondogo,  huku wakiwashauri wahusika kurudi katika mstari wa maadili ya vyombo vyao vya habari.

“Sio kwamba makosa hayapo na sio kwamba changamoto hazipo lakini Wizara ya Habari tumeamua kuitikia wito wa Rais wa kutekeleza zile R4 ikiwemo Turidhiane, tuvumiliane, tujenge upya pamoja,” anasema Waziri Nape.

Akizungumzia katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Mwananchi Communication Ltd (MCL), Bakari Machumu amesema vyombo vya habari vinapongeza hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali za kuhahakisha vyombo vya habari vinakuwa huru lakini kwa kuzingatia weledi zaidi.

 “Tunapongeza  hatua hiyo, lakini inafaa sasa twende mbali zaidi kuangalia sheria, taratibu na kanuni zinasemaje ili kuona pia ni kwa kiasi gani ina msukumo zaidi katika uwekezaji, na  inasaidiaje kuviinua kiuchumi vyombo hivi vya habari,” amesema Machumu.

Amesema ili vyombo vya habari viweze kuwapa waandishi wa habari ajira ya kudumu na mikataba,  ni lazima viwe na uwezo wa kujiendesha.

Amesema bila hivyo bado vitakuwa vinahangaika tu, hivyo Serikali  lazima iweke uwezeshaji wa kimazingira kwa sekta binafsi ili malengo hayo yawe na tija.

“Sisi kama sekta binafsi kwa hatua hii ambayo Serikali imeonyesha inatutia moyo kwamba hili tunaliweza na lazima twende mbele pamoja na tuko tayari kwenda pamoja,” amesema.

Awali, Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Khamis Abdulla,  amesema katika kuboresha sekta ya habari, wizara imeendelea kufanya mapitio ya Sera ya Habari na Utangazaji ya mwaka 2003 na inakaribia kukamilisha rasimu ya mkakati wa uchumi wa kidigitali na mkakati wa Taifa wa mawasiliano.

Naye Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi amesema ili kuimarisha sekta ya habari, Serikali iko katika mapitio ya vyuo vinavyozalisha waandishi wa habari,  kwa lengo la kuona namna vinavyokidhi kuzalisha wataalamu wazuri wanaokuja kuhudumu katika sekta hiyo baada ya masomo.

“Lengo ni kuona Taifa baadaye linakuwa na waandishi waliobobea katika masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano kuanzia huko vyuoni wanapotoka,” amesema Matinyi.