Nape ataka ufanisi taarifa makosa ya mitandao

Muktasari:

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ametoa vifaa vya Tehama kwa Jeshi la Polisi na Ofisi na Mwendesha Mshtaka wa Serikali (DPP) ili kuleta ufanisi katika kushughulikia taarifa za makosa ya mtandao.

Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, amesema mfumo wa uhakiki, utunzaji wa kumbumbuku za makosa ya mtandao utasaidia kuharakisha upelelezi wa makosa ya mtandao na kupunguza muda wa kuyashughulikia.

Nape ambaye ni Mbunge wa Mtama mkoani Lindi, amesema mfumo huo utasaidia pia kuharakisha upatikanaji wa ushahidi wa makosa ya mtandao.

Waziri huyo, ameeleza hayo leo wakati wa akigawa vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), vilivyotolewa na wizara yake kwenda kwa Jeshi la Polisi na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP) kwa ajili ya kutumika kwenye moduli ya makosa ya mtandao.

Nape amesema kumekuwapo na changamoto za takwimu zinazohusu makosa ya mtandaoni baina ya taasisi na wadau, hatua inayosababisha ugumu wa kupata uhalisia wa mwendelezo wa matukio tangu kupokelewa kwa taarifa, kushughulikiwa na namna yanavyoendelea kufanyiwa kazi.

"Kukamilika kwa moduli hii kutatua changamoto kwa taasisi zote zinazoshughulika na makosa ya mtandao ambapo zitakuwa zikitumia mfumo mmoja badala ya mifumo tofauti iliyokuwapo.

"Suala hilo litaharakisha upelelezi wa makosa ya mtandao na kupunguza muda wa kuyashughulikia, ukiangalia mwenendo wa makosa ya mtandaoni sio makubwa lakini yana ongezeka lazima tuchukue hatua ya kuyadhibiti," amesema Nape.


Amefafanua kuwa wizara yake itazungumza na watu mahakama ili kuangalia namna ya kushughulikia kwa uharaka kesi za makosa ya mtandao.

Nape amesema hatua ya Polisi, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Ofisi ya DPP kutumia mfumo mmoja utarahisisha mchakato wa utoaji wa haki, ambao  ni pamoja na kuifuatilia na kupata mrejesho kwa urahisi.

"Kama mtu ataweza kuripoti tatizo nikiwa nyumbani badala ya polisi imerahisisha kufikisha changamoto kwa wakati sahihi kwa mamlaka husika," amesema Nape.

Amesema Tehama, yameongezeka kwa kasi kubwa nchini, wizara inapotunga sheria lazima iwawezeshe wale wanaoitekeleza ili usimamizi wa mchakato huo uwe  ufanisi zaidi na anga la mtandao litakuwa usalama zaidi.


Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka, Joseph Pande amesema, "siku zote mtoa taarifa wa matukio ya mtandao wanapenda kupata mrejesho na kujua hatua ya jambo waliowasilisha polisi.Lakini sasa hivi wakisharipoti wanakuwa na ugomvi na mpelelezi wakitaka awajulishe.

"Lakini kupitia mfumo huo mlalamikaji atapata taarifa ya mwenendo wa kesi yake hata akiwa nyumbani, watajua kesi yao ipo kituo gani cha polisi na namna ya inavyoshughulikiwa hadi kufikishwa mahakamani," amesema Pande.

Naye Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IJP), Camillius Wambura ameishukuru wizara hiyo kwa vifaa hivyo zikiwemo kompyuta za mpakato na mezani zitakazotumiwa polisi na pamoja na ofisi ya mwendesha mashtaka, akisema vitarahisisha katika utekelezaji wa majukumu yao.

"Nikuhakishe Waziri sasa hivi polisi inapitia katika mfumo wa mabadiliko, tumeanza na mabadililo ya kimaadili, nidhamu na utendaji kazi, vifaa hivi itakwenda kutumika kwa kazi iliyokusudiwa.

"Usiwe na wasiwasi vifaa hivi vitakwenda kufanya kazi, tumekubaliana ndani ya jeshi tuongee kidogo na tutendee zaidi ili kutoka na matokeo makubwa," amesema Wambura.