Nape atishia kushikilia shilingi ya Profesa Maghembe

Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye

Muktasari:

Nape akerwa na mifumo ya wizara hiyo

Dodoma. Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye ametishia kushikilia shilingi ya mshahara wa Waziri wa Maliasi na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe.

Akichangia bajeti ya wizara hiyo, Nape ambaye aliwahi kuwa wiziri katika baraza la mawaziri wa Rais John Magufuli ameitaka Serikali kutengua zuio lake la kusafirisha viumbe hai kwenda nje, baada ya Serikali kuonyesha wafanyabiashara hao hawakuwa na makosa na ndio maana inataka kulipa kifuta jasho.

“Serikali iruhusu wasafirishe hao viumbe hao ambao walikwishawakamata,wakawaweka kwenye mazizi yao kwa kufuata utaratibu, walikata leseni, walilipa kodi na wengine walichukua mikopo benki.”

“Na  wengine walishalipwa pesa za utangulizi kabla ya kupeleka hao wanyama nje. Mimi nilidhani badala ya kuzungumza kifuta jasho hapa izungumzwe habari ya fidia watu wamepata hasara.”

“La pili uamuzi huu utenguliwe na mheshimiwa Waziri niko tayari kushika shilingi yako ili utengue uamuzi huu. Hawa watu hawa kwa kweli hawakustahili kuadhibiwa,”amesisitiza  Nape.

Nape amesema hata kulipotokea matatizo katika muwindaji, Serikali haikuwaadhibi watu wote walioko katika sekta hiyo bali wale tu waliofanya makosa hivyo, katika suala la wanyama nalo liwe hivyo.