Nape atoa siku saba waajiri kulipa madai ya marehemu

Muktasari:

Serikali imetoa siku saba kwa waajiri wote wanaodaiwa na waandishi wa habari waliofariki katika ajali ya gari wilayani Busega kulipa stahiki zao.

Mwanza. Serikali imetoa siku saba kwa waajiri wanaodaiwa na waandishi wa habari waliofariki katika ajali ya gari wilayani Busega kulipa stahiki zao.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye wakati shughuli ya kuaga na kutoa heshima za mwisho kwa waandishi watano na dereva wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza waliofariki dunia jana.

"Nimepewa salamu hapa kuwa miongoni mwa waliolala kwenye majeneza hapa mbele yangu hawajalipwa stahiki zao; natoa siku saba kwa waajiri wote wanaodaiwa kulipa stahiki zote za marehemu na kutoa taarifa ofisi ya mkuu wa mkoa," ameagiza Nape

Akionyesha msisitizo kuhusu agizo hilo, Waziri huyo aliwataka wamiliki wa vyombo vya habari waoadaiwa kutambua kwamba wizara yake ndiyo imeshikilia leseni zao.

"Yawezekana kuna hali ngumu ya kiuchumi, lakini nasema stahiki zote za marehemu hawa zilipwe ndani ya siku saba. Hayo ya hali ngumu tutayazungumza huko mbeleni kwa waandishi ambao wako hai ila kwa hawa marehemu lazima walipwe," ameagiza Waziri Nape

Awali, wawakilishi wa waandishi wa habari waliotoa salamu walimuomba waziri huyo kushughulikia changamoto ya waandishi kutolipwa stahiki zao huku wakifichua kuwa baadhi ya marehemu hawajalipwa kwa miaka miwili iliyopita.

🔴#LIVE: Miili ya wanahabari watano na dereva ikiagwa

Waliozungumza kwa niaba ya wanahabari ni Mwenyekiti wa Kluabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC), Edwin Soko na Mkurugenzi mtendaji wa Klubu ya Waandishi wa Habari (UTPC), Abubakar Karsan.