NCCR Mageuzi yaungana na Chadema, ACT kususia mkutano wa Msajili

Monday October 18 2021
Mkutano pc
By Tuzo Mapunda

Dar es Salaam. Chama cha NCCR- Mageuzi kimetoa hoja tatu za kususia mkutano ulioitishwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini (ORPP) ikiwemo ya kutoshirikishwa katika maandalizi na kutokuwepo kwa uwazi.

Mkutano huo umepangwa kufanyika Dodoma Oktoba 21 hadi 23, 2021 na  utahusisha wadau watatu ambao ni Jeshi la Polisi, vyama vya siasa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa lengo likiwa ni kujadili na kuondoa mvutano baina  ya vyama vya siasa na jeshi la polisi.

Chama hicho kimendeleza na msimamo huo uliotolewa kwa mara ya pili na kikiungana na ACT-Wazalendo na Chadema vilivyotoa msomo kama huo.

Akizungumza Dar es Salaam leo Oktoba 18, Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia amesema kuwa, Ofisi ya ORPP ni watuhumiwa katika hilo hivyo hawawezi kujipa kazi ya unyapara usuluhishi kwani hakuna mahali imeweza kutekeleza wajibu wake wa kisheria.

“Ofisi ya Msajili wa Siasa na Jeshi la Polisi ambao ndiyo watuhumiwa wakubwa walikutana na kutoa msimamo wa kupotosha umma kwamba eti kunaupungufu wa sheria? Kazi ya Polisi ni kusimamia sheria zilizopo,” amesema Mbatia.

Amesema mkutano huo ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kimsingi na mpangilio  hauna nia njema bali kufifisha na kubeza hoja  zao halali za kuhakikisha taifa linakuwa na mfumo imara na wenye utu.

Advertisement

Mbatia ameeleza kwamba msimamo huo kutoshiriki unatokana na kikao cha ndani kilichofanyika jana Oktoba 17, 2021 na badala yake watazungumza na wadau wengine wa demokrasia ikiwemo vyama vingine vinavyoathiriwa unyanyasaji ili kupata suluhisho la pamoja.

Advertisement