NCCR yasema uchumi wake hauruhusu kufanya mikutano

Joseph Selasini


Muktasari:


  • Viongozi wa NCCR Mageuzi wametakiwa kurudi majimboni kuhimizawananchi kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa.

Dar es Salaam. Viongozi wa Chama cha NCCR Mageuzi wametakiwa kurudi majimboni mwao ili kuwahamasisha wananchi kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa na kukijenga chama.

Hatua ya chama hicho imekuja baada ya kile kinachoelezwa hali ya uchumi wa chama hicho kutowaruhusu kufanya  mikutano ya hadhara kama vyama vingine.

Kuwaambia viongozi wao warudi majimboni ni moja ya mikakati yao kukabiliana na hali hiyo ya kiuchumi.

Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Tanzania Bara, Joseph Selasini ameiambia Mwananchi Digital leo Aprili 19, 2024 kwamba kila kiongozi ametakiwa kurudi kwenye jimbo lake kwa lengo la kuendelea kukijenga chama, kuwahamasisha wananchi kipindi hiki wanapojiandaa kwa uchaguzi wa Serikali za mitaa.

Selasini amesema, chama chao hakijajiimarisha kiuchumi ili kumudu kufanya mikutano ya hadhara.

“Kama ni kiongozi wa Kamati Kuu au Halmashauri Kuu, tumekubaliana kila mmoja arudi kwenye eneo lake kuongeza nguvu,  kuhamasisha wananchi, lakini pia kushiriki kusimamia wagombea kwenye chaguzi zetu za ndani ambazo sasa tunafanya katika ngazi ya mitaa na vijiji,” amesema.

Amesema, NCCR hakiwezi kufanya mikutano ya hadhara kutokana na uchumi wa chama kutokuwa vizuri, lakini wanaendelea na harakati za kukijenga kwa njia hiyo ya kila kiongozi kurudi kwenye jimbo lake.

“Tunajipanga kwa njia tofauti, watu hawatuoni tukifanya mikutano ya hadhara kwa sababu ya hali yetu ya kiuchumi kutoturuhusu kufanya hivyo. Inafahamika kwa kiasi kikubwa hii mikutano ya hadhara inategemea uchumi wa chama,” ameongeza kuwa.

 Amesema, kingine walichokubaliana ni viongozi kusimamia ili wagombea kwenye ngazi ya vijiji na vitongoji wapatikane na kila kiongozi wa NCCR hivi sasa yupo kwenye eneo lake kukamilisha harakati hizo.