Nchimbi aonya makada CCM wanaotukana watumishi serikalini

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuael Nchimbi

Muktasari:

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi(CCM), Dk Emmanuael Nchimbi ni kama ametupa ‘jiwe gizani’ akiwaonya baadhi ya viongozi wa chama hicho wanaotumia mamlaka yao kudhalilisha viongozi wa Serikali. 

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuael Nchimbi ni kama ametupa jiwe gizani akiwaonya baadhi ya viongozi wa chama hicho wanaotumia mamlaka yao kudhalilisha viongozi wa Serikali. 


Bila kutaja majina, Dk Nchimbi amesema kumekuwa na utamaduni wa viongozi wa chama hicho kutoa maelekezo kwa viongozi wa Serikali.

 
Akizungumza leo Januari 20, 2024 jijini Dar es Salaam wakati wa mapokezi yake baada ya kuchaguliwa kushika nafasi hiyo, Nchimbi amesema hakuna mtu asiyejua CCM ndio chama kinachoongoza Serikali, hivyo hakuna ulazima wa kutumia nguvu kudhalilisha watumishi wake.


Januari 15, mwaka huu, chama hicho kilitangaza kumteua Nchimbi aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Misri kushika nafasi hiyo iliyokuwa wazi baada ya Daniel Chongolo kujiuzulu kwa madai ya kuchafuliwa kwenye mitandao ya kijamii. 


“Chama chetu kisikwepe wajibu wake wa kuisimamia Serikali, ni wajibu wa kikatiba na kikanuni. Sisi ndio tulichaguliwa na wananchi. Mkataba ni kati ya CCM na wananchi na mtekelezaji wa mkataba ni Serikali, lakini tusimamie bila kuwa na kiburi, tusimamie kwa weledi,’’ amesema. 


Bila kutaja jina la mhusika anayetukana viongozi wa Serikali, Nchimbi alisema: “Hatuwezi kusimamia Serikali kwa kuwa tunawatukana tukana watu, wewe hapa, kwa nini, mshenzi sana wewe, ahaa hiyo mshenzi haipo katika Ilani ya CCM , lazima tuwaheshimu watumishi wa Serikali, tuongoze kwa weledi.” 


Tukio la mapokezi lilifanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja kwa shamrashamra mbalimbali zilizoongozwa na burudani kabla na baada ya hotuba yake iliyotumia wastani wa dakika 10.


 “Kila mtu anafahamu kwamba CCM ndio inayotawala,  hatuhitaji kubeba rungu kubwa kuonyesha kwamba sisi ndio tunatawala na tunatawala kwa niaba ya wananchi, kwa hiyo viongozi wa CCM msione haya kusimamia. Lakini tusimamie kwa weledi,” amessema Nchimbi.


Kuhusu ujenzi wa chama, Dk Nchimbi ameahidi kushirikiana na viongozi wa chama hicho kuhakikisha kinaendelea kuaminiwa na Watanzania katika chaguzi zijazo.


Amesema anaamini katika falsafa ya vitendo zaidi kuliko maneno mengi, huku akisisitiza kujipanga kwa ajili ya ushindi wa kishindo kwenye chaguzi hizo.


Wakizungumzia ujio wake, Katibu mwenezi wa CCM Wilaya ya Ilala, Mwinyimkuu Sangaraza amesema Nchimbi amebeba matumaini ya chama hicho kwenye chaguzi kutokana na uwezo wake.


“Maagizo yake ni faraja, tunaamini atatusaidia kuimarisha zaidi chama na chaguzi zijazo tutashinda kwa kishindo,” amesema Sangaraza. 


Kwa upande wake, Diwani wa Viti Maalumu (CCM) kutoka Wilaya ya Temeke, Mwadunia Zama amesema uteuzi wa Nchimbi ni salamu kwa vyama vya upinzani nchini kuelekea chaguzi zijazo.

 
“Hatutaongea kwa kutumia nguvu sana, bali kwa ushawishi wake pamoja na kazi alizofanya mama (Rais Samia Suluhu Hassan),” amesema.