Ndalichako awataka waongoza watalii nchini kuwa mabalozi
Arusha. Waziri wa Kazi, Ajira, Vijana na wenye ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako amewataka waongoza watalii nchini kuwa mabalozi wazuri katika kutangaza vivutio vya utalii sambamba na kuwapeleka watalii kujionea vivutio hivyo ili kuweza kufurahia neema ya kipekee iliyopo katika nchi yetu.
Hayo yamesemwa leo Juni 17, 2023 jijini Arusha wakati akifunga mafunzo ya kukuza ujuzi kwa waongoza watalii yaliyoandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kazi, Ajira, Vijana na wenye ulemavu kwa kushirikiana na TTGA yaliyofanyika kwa muda wa siku sita jijini hapa.
Ndalichako amesema ni jukumu la waongoza watalii kuhakikisha wanatangaza vivutio hivyo kwa wageni mbalimbali wanaofika nchini ili kuongeza idadi ya watalii watakaotembelea vivutio hivyo kwa wingi na hatimaye kuongeza pato la Taifa.
Aidha amewataka kutoa huduma nzuri kwa watalii hao na kuwa wakarimu pamoja na kutumia lugha nzuri ili sekta ya utalii iendelee kukua zaidi na kuwashawishi watalii kuendelea kutembelea kwa wingi vivutio vyetu.
Aidha amewataka waajiri nchini kuhakikisha wanatii sheria za kazi bila shuruti ikiwemo kulipa mishahara ya wafanyakazi wao kwa wakati kwani serikali ina dhamira ya dhati kuhakikisha wafanyakazi wanafanya kazi kwa weledi.
"Utekelezaji wa mafunzo haya ya kukuza ujuzi kwa wafanyakazi ni muhimu sana na yatakuwa endelevu kwani ni lazima muwe na ujuzi stahiki wa kuongoza watalii vizuri kwani nyie ndio mnaokuwa na wageni hao muda mwingi na hivyo mna kila sababu ya kutumia ujuzi wenu ipasavyo kuhakikisha mnawaridhisha watalii hao," amesema Profesa Ndalichako
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa TPSF, Raphael Maganga amesema kuwa utoaji mafunzo hayo kwa waongoza watalii hao utasaidia sana kuwa mabalozi wazuri katika utendaji kazi wao na kuongeza idadi ya watalii na kuweza kufikia malengo yaliyowekwa .
Maganga amesema sekta ya utalii inaendelea kukua sana na inaendelea kuajiri zaidi ya Watanzania milioni 1.5 ikiwa ni sekta inayoajiri watanzania wengi sana.
"Taasisi ya sekta binafsi Tanzania (TPSF) tunaendelea kushirikiana na serikali katika kuhakikisha makampuni ambayo hayatoi mikataba yanafuatiliwa ili watu waweze kupata haki zao za msingi," amesema
Mwenyekiti wa Chama cha Waongoza Watalii Tanzania (TTGA), Lembris Loipuko amesema jumla ya waongoza watalii 696 kutoka kanda ya kaskazini wameweza kupata mafunzo hayo ambapo mada mbalimbali zimetolewa ikiwemo huduma kwa wateja, huduma ya kwanza ya kisasa, utangulizi wa huduma ya uongozi wa watalii wandani .
Amesema kupitia mafunzo hayo wataweza kuyafanyia kazi yale yote waliyojifunza ili kuunga juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan ya kukuza utalii nchini pamoja na juhudi za serikali za kufikia watalii milioni 5 ifikapo mwaka 2025.
Aidha amesema pamoja na mafanikio mbalimbali, wameomba serikali iwasaidie kuwa na vifurushi rafiki kwa waongoza watalii kwani wanasikitishwa sana na serikali kusitisha huduma na kukataa kuhuisha vifurushi vya Bima ya Afya kupitia NHIF ambavyo waongoza watalii walikuwa wanufaika.
Aidha waliomba serikali kuwapatia gari la kutoa msaada kwani kwa upande wa Mlima Kilimanjaro halipatikani kwa wakati jambo linalopelekea kuhatarisha maisha ya wageni na wapanda mlima kwa ujumla.