Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wateja benki zilizofungwa walipwa Sh9.07 bilioni

Muktasari:

  • Kupitia Bodi ya Bima ya Amana (DIB) sasa mteja mwenye amana ya Sh7.5 milioni kushuka chini anaweza kupata fedha zake mara moja ikiwa benki anayotumia ikifilisika.

Dar es Salaam. Zaidi ya Sh9.07 bilioni zimelipwa kwa wateja waliokuwa na amana katika benki saba zilizofungwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kufuatia kufilisika kwa taasisi hizo za kifedha.

Fedha hizo zimetolewa tangu Bodi ya Bima ya Amana (Deposit Insurance Board – DIB) ilipoanza rasmi utekelezaji wa majukumu yake mwaka 1994 hadi kufikia Machi mwaka huu.

Hayo yameelezwa leo Julai 2,2025 na Mkurugenzi wa bodi hiyo, Isack Kihwili alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya maonyesho ya 49 ya biashara ya kimataifa, maarufu Sabasaba.

Kihwili amesema kiwango hicho cha malipo kimegusa wastani wa asilimia 75.76 ya jumla ya fidia zote zinazostahili kulipwa.

Amesema miongoni mwa waliolipwa ni wateja wa benki zilizofungwa, zikiwemo FBME Bank, ambayo tayari zaidi ya asilimia 57 ya fidia zake imelipwa, Covenant Bank asilimia 83.73, Kagera Farmers’ Cooperative Bank asilimia 94.06), Meru Community Bank asilimia 92.35, Mbinga Community Bank asilimia 84.66, Njombe Community Bank asilimia 87.26, pamoja na Efatha Bank, ambayo bado inaendelea kufanyiwa tathmini ya fidia.

“Wateja ambao bado hawajalipwa ni wale tu ambao hawajawasilisha madai yao. Tunawashauri wafike haraka na kuwasilisha nyaraka zao ili waweze kulipwa stahiki zao,” amesema Kihwili.

Bodi hiyo, iliyoanzishwa rasmi mwaka 1991, awali ilikuwa chini ya usimamizi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), lakini kwa sasa inajiendesha kama taasisi huru.

Hadi kufikia Desemba 2024, bodi hiyo ilikuwa na mtaji wa Sh1.3 trilioni, ikiwa ni matokeo ya kuongezeka kwa idadi ya taasisi za fedha zinazochangia, pamoja na maboresho katika mifumo ya usimamizi na uendeshaji.

“Kwa sasa tuna jumla ya wachangiaji 42 ambao ni benki yaliyosajiliwa na BoT, na huchangia asilimia 0.15 ya amana kwa mwaka kama michango ya bima,” amesema.

Amesema kiwango cha fidia kwa kila mteja kilikuwa wastani wa Sh250,000 mwanzoni, lakini kimeongezeka hadi Sh1.5 milioni mwaka 2010, na kufikia Sh7.5 milioni tangu mwaka 2023.

Hii ina maana kwamba endapo benki itafungwa kwa sasa, mteja mwenye amana ya hadi Sh7.5 milioni atalipwa fidia kamili mara moja.

“Kama mteja ana zaidi ya Sh7.5 milioni, bodi itafuata taratibu nyingine za usimamizi wa mali za benki hiyo kwa mujibu wa sheria za ufilisi,” amesema.

Kwa mujibu wa takwimu, zaidi ya asilimia 99.24 ya wateja wa benki zote nchini wamekingwa na mfumo huu wa bima ya amana, kiwango ambacho kiko juu ya kiwango cha kimataifa kinachotakiwa cha asilimia 90.

Hata hivyo, alikiri kuwapo kwa changamoto kwa wateja wa benki zilizo na matawi au ushirikiano na taasisi kutoka nje ya nchi, kutokana na utofauti wa mifumo ya kisheria na kifedha.