Ndani ya Habari: Kizungumkuti wasafirishaji haramu wa mkaa

Kibaha. Licha ya Serikali kupiga marufuku usafirishaji wa mkaa kwa pikipiki maarufu kwa jina la busta, agizo hilo limeendelea kukumbana na changamoto katika utekelezaji, baada ya wasafirishaji hao haramu wa mazao hayo ya misitu kuendelea na shughuli hiyo.

Wasafirishaji hao wamekuwa wakitumia barabara kuu na njia zisizo rasmi kuupeleka Dar es Salaam na maeneo mengine mkoani Pwani.

Novemba 9, 2022 Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge wakati akitoa taarifa kwa Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango juu ya hatua mbalimbali zinazochukuliwa na mkoa huo ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan yanayolenga kuondoa changamoto ya upungufu wa maji kwenye Bonde la Mto Ruvu unaosababishwa na shughuli za kibinadamu, alisema wameazimia kudhibiti pikipiki zinazobeba mkaa kwa kuzisajili na kuzifuatilia kujua zinakotoa mkaa.

Kunenge alisema mkoa huo unapanga kuja na mpango wa kudhibiti uvunaji wa mkaa kwa kupunguza utoaji vibali vya mkaa, ili kuhamasisha matumizi ya nishati ya gesi majumbani.

Hata hivyo, ikiwa ni takriban miezi mitano, shughuli za uvunaji miti katika misitu ya vijiji vya Kimala Masale na Madege wilayani hapa, bado zinaendelea, huku usafirishaji wa mkaa kwa pikipiki ukiendelea kama kawaida.

Licha ya mkoa kujipanga kukabiliana na uharibifu wa misitu na usafirishaji haramu wa mkaa, Mwananchi limeshuhudia shughuli hizo zikifanyika katika vijiji hivyo, ingawa hivi karibuni ilifanyika operesheni ya kuwaondoa wavunaji na wachoma mkaa.


Wasemavyo viongozi, wananchi

Wenyeviti na wananchi wa vijiji hivyo kwa nyakati tofauti, wamesema uchomaji mkaa na usafirishaji unaendelea, na kwamba wanaofanya hivyo wengi wao wanaotoka nje ya maeneo hayo, huku nguvu ya kukabiliana nao ikiwa ni ndogo.

“Hali si nzuri, maeneo yote unayoyaona yanatuzunguka yalikuwa na miti mingi mikubwa, lakini kwa sasa hakuna. Ndio maana hata vyanzo vya maji vimekauka. Uharibifu wa msitu ni mkubwa,” anasema Mwenyekiti wa Kijiji cha Kimala Masale, Salum Mtego akisisitiza katika kuomba mamlaka za juu za nchi zitoe tamko la kupiga marufuku uvunaji miti.

Mtego anasema wanategemea zaidi msaada wa doria ambazo hufanywa na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS). Anasema pamoja na ombi la kupigwa marufuku uchomaji mkaa, pia wanaitaka Serikali kuiongezea nguvu taasisi hiyo kwa kuipa vifaa na askari usu.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Madege, Idd Salum anasema shughuli ya uchomaji mkaa imeharibu mandhari ya kijiji chao ambacho kilisifika kwa uoto asili uliolipendesha eneo hilo.

“Lakini wimbi la kukata miti ili kuchoma mkaa lilipokuja, tena watu wengi walitoka nje ya hapa mambo yaliharibika, maana miti imebaki hii midogo midogo tu,” anasema.

Wakizungumzia hali hiyo, baadhi ya wakazi wa vijiji hivyo wanaitaka Serikali kuwapelekea shughuli mbadala nje ya biashara hiyo na kilimo ambacho wanadai kimeathiriwa na mvua kutonyesha kwa wakati.

“Mfano Serikali ituletee mikopo ya riba nafuu na pia itusaidie kuzifikia fursa nyingine, hii miti michache iliyopo hakuna atakayeisogelea (kuikata) awe wa hapa (kijijini) au kutoka nje ya eneo hili,” anasema Salehe Lujo, mkazi wa Madege huku Salma Fundi akitaka kinamama waanzishiwe miradi ya kuwakwamua kiuchumi ili waweze kuwa na ushawishi kwa wanaume kuachana na uchomaji mkaa.

“(Awali) sisi tuligoma wasikate miti, lakini kuna watu walikuwa wanakuja kutoka mbali kukata, lakini kama na sisi (wanawake) tukiwezeshwa (kwa kuanzishiwa miradi ya kiuchumi) ina maana tutaongeza ushawishi kwa waume zetu kupinga hiyo kazi,”anasema.

Hamidu Mzome wa Kijiji cha Kimala Masale anasema upigaji marufuku wa uchomaji mkaa unafaa kuanzia ndani ya familia - kwa wazazi kubeba jukumu hilo ili kulisaidia Taifa kuepuka kugeuka jangwa, kwa sababu wanawajibika na makuzi ya watoto na pia ustawi wa maisha na maeneo wanayoishi.

“Tukisema liwe ni jukumu la Serikali peke yake hatutafanikiwa. Mfano nyumbani kwangu vijana nilishawaambia wafanye shughuli nyingine, lakini sitaki kusikia mtu anachoma mkaa,” anasema.


Kauli ya TFS

Kaimu kamanda wa TFS Kanda ya Mashariki, Mathew Ntilicha anasema licha ya kutoa elimu kwa wafanyabiashara na wasafirishaji wa mkaa kuhusu sheria ya misitu na biashara ya mkaa, lakini wameanza kukutana nao mara kwa mara kwa ajili ya utekelezaji wa maelekezo ya mkuu wa mkoa.

“Kwa sasa tunaamini kwamba hili suala (la biashara haramu ya mkaa) linakwenda kumalizika,” anasema Ntilicha.

Hata hivyo, anasema kwa sasa kuna kesi saba zinazohusisha watuhumiwa 45 na kwamba kesi mbili ziko mahakamani na tano ziko polisi kwani upelelezi unaendelea.

“Pia tumekubaliana (na viongozi wa chama cha bodaboda) kurejesha uoto kwa kupanda miti katika maeneo ambayo yameathirika katika vijiji husika,” anasema.

Akizungumzia suala la wananchi kuwezeshwa ili waachane na shughuli za ukataji miti kwa ajili ya mkaa, Ntilicha anasema kuna Mfuko wa Misitu ambao upo kwa ajili ya kutoa ruzuku kwa watu wenye nia ya kujikita katika shughuli za ufugaji nyuki na upandaji miti.

“Anaweza akawa mtu mmoja au kikundi wakaandika andiko kwa ajili ya uhifadhi na wanaweza wakaandika andiko la miradi ya upandaji miti na ufugaji nyuki, au wakaanzisha shughuli ya upandaji miti ya matunda wakapata fedha,” anasema.


Mwongozo na sheria

Mwongozo wa uvunaji mazao ya misitu wa mwaka 2017 unaelekeza biashara hiyo kufanyika kwa kuzingatia sheria na taratibu, ikiwamo kila anayetaka kuvuna miti kwa shughuli ya kibiashara kuwa na leseni inayotolewa na kamati ya usimamizi wa uvunaji misitu ya wilaya.

Pia, mwongozo unaelekeza kila msafirishaji kufanya hivyo kati ya saa 12 asubuhi hadi saa 12 jioni na kila anayefanya hivyo ni lazima asimame katika vituo vya ukaguzi.

Hata hivyo, takwimu zinaonyesha moja kati ya makosa yanayojirudia ni leseni kutumika hata baada ya muda wa ukomo na au kuzidisha kiasi cha magunia kinachoruhusiwa kwa mujibu wa leseni ya usafirishaji. Uzito wa gunia la mkaa unaoruhusiwa kusafirishwa kisheria ni kilo 50.

Kuhusu mkaa, Sheria ya Misitu Na14 ya 2002, inaeleza kuwa kila anayepatikana na kosa la kuchoma mkaa kinyume cha sharia atalipa faini isiyozidi Sh1 milioni au kwenda jela miaka miwili ama adhabu zote mbili.

Lakini kifungu cha 89(a) cha sheria hiyo kinakazia kuwa adhabu inaweza kwenda mbali zaidi kwa mshtakiwa kufungwa hadi miaka saba na pia mkaa aliokamatwa nao kutaifishwa.

Sheria hiyo pia inazuia ununuzi wa mkaa uliopatikana kinyume cha sheria na adhabu na anayepatikana na kosa hilo sambamba na wanaohifadhi faini yake ni Sh5 milioni au jela miaka miwili ama adhabu zote mbili kwa pamoja.