Ndege iliyozama Ziwa Victoria yatolewa

Ndege ya Precision Air iliyopata ajali Ziwa Victoria Novemba 6, 2022 na kusababisha vifo vya watu 19 na majeruhi 24 ikitolewa kwenye maji.
Muktasari:
- Ndege hiyo ambayo ilizama kwenye maji karibu na Uwanja wa Ndege wa Bukoba mkoani Kagera Novemba 06, 2022 ilisababisha vifo vya watu 19 huku wengine 24 wakinusurika.
Bukoba. Ndege ya Precision Air iliyosababisha vifo vya watu 19 na majeruhi 24 baada ya kupata ajali Ziwa Victoria imetolewa kwenye maji.
Ndege hiyo ambayo ilizama kwenye maji karibu na Uwanja wa Ndege wa Bukoba mkoani Kagera Novemba 06, 2022 imetolewa leo Jumanne Novemba 08 kwa msaada wa mitambo kutoka Mgodi wa Madini ya Dhahabu Geita (GGM).
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema ndege hiyo imetolewa kwenye maji na kuwekwa kwenye eneo la ndege kubwa zinapopita kwenda kutua uwanjani hivyo itaondolewa ili kupisha ndege hizo.
"Ndege hiyo imetolewa kwenye maji kwa msaada wa mitambo kutoka Mgodi wa Madini ya Dhahabu Geita (GGM) na ilipowekwa ndege ni eneo la ndege kubwa zinapopita hivyo itaondolewa ili kupisha ndege hizo" Amesema Msigwa
Hata hivyo, Mwananchi ilimtafuta Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Bukoba kuzungumzia kuondolewa kwa ndege hiyo bila mafanikio.
Ndege hiyo ambayo ilikuwa inatoka Dar es Salaam kwenda Bukoba ilisababisha vifo vya watu 19 na wengine 24 waliokuwa kwenye ndege hiyo wakinusurika.
Hata hivyo, jana miili ya watu 19 iliagwa katika uwanja wa Kaitaba kabla ya kukabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya taratibu za mazishi.
Pia, Msigwa amebainisha kuwa timu tatu zinatarajia kufanya uchunguzi ajali ya ndege hiyo.