Ndugai atia neno kukatika umeme

Muktasari:

  • Wakati maeneo mbalimbali nchini yakiendelea na machungu na mgawo wa umeme pamoja na katika katika ya umeme, Spika wa Bunge Mstaafu Job Ndugai amezungumza kero hiyo.

Dodoma. Spika wa Bunge Mstaafu Job Ndugai, ameitaka Serikali kuboresha taratibu zake katika kuwahudumia wananchi ikiwemo kutenga fedha za kutosha kutekeleza miradi, huku akionyesha kukerwa na kukatika kwa umeme.

Ndugai ambaye pia ni Mbunge wa Kongwa, ameyasema hayo wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma, iliyotembea na kukagua miradi mbalimbali ambapo amesema kukatika umeme kunarudisha nyuma nyuma jitihada za wananchi katika kujiletea maendeleo kupitia viwanda mbalimbali vya uzalishaji.

 "Tanesco (Shirika la Umeme Tanzania) ni lazima mwende na nia aliyonayo Mheshimiwa Rais, baadhi ya desturi zenu lazima zibadilike ili muepushe kero hizi kwa wananchi," ameonya Spika huyo Mstaafu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kongwa, mkoani Dodoma.

Aidha kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumatano Novemba 15, 2023 na kitengo cha mawasiliano cha mkoa wa Dodoma, Ndugai amesema ni jambo muhimu kwa serikali kutenga fedha zinazotosheleza kutakidhi mahitaji ya wananchi.

“Tunashukuru jitihada za Serikali za kuwaletea Wananchi Maendeleo. Wito wangu kwa Serikali Kuboresha taratibu zake katika kuhudumia Wananchi ikiwemo kutenga fedha zinazojitosheleza kutekeleza miradi mbalimbali ili kukidhi mahitaji ya wananchi,” amesema.

Naye Katibu wa CCCM Mkoa wa Dodoma, Pilli Mbaga amepongeza wilaya hiyo kwa kutekeleza Ilani ya CCM ya mwaka 2020 hadi 2025 na kuwataka wananchi kuendelea kuiamini Serikali ya Awamu ya Sita.

“Tunawapongeza kwa kazi nzuri iliyofanyika. Wananchi tuendelee kuiamini Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais wake Samia Suluhu Hassan, kwani imedhamiria kutatua kero zinazowakabili wananchi,” amesema.

Aidha, Mbaga amewataka madaktari na wauguzi kuwa na kauli nzuri kwa wagonjwa ili kutimiza dhamira nzuri ya Serikali ya kutoa huduma bora kwa wananchi wake.

Katika ziara hiyo, kamati ya Siasa ya Mkoa imetembelea na kukagua miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa barabara ya kiwango Cha lami ya Mwalimu Nyerere yenye urefu wa Kilometa moha ambayo imejengwa kwa tamani ya Sh487.19 milioni.

Miradi mingine ni ujenzi wa Miundombinu katika Hospitali ya Wilaya wenye thamani ya Sh4.64 bilioni unaohusisha wodi tatu za wagonjwa na jengo la mama na mtoto na kisima cha maji katika Kijiji Cha Laikala "B" wenye thamani ya Sh780.56 milioni, Shule ya Msingi Moleti iliyojengwa kwa thamani ya Sh318.8 milioni.

Mradi mwingine ni kuboresha umeme kwa ajili ya kutatua kero ya umeme hafifu kwa Wilaya za Kongwa, Mpwapwa mkoani Dodoma na Gairo iliyopo mkoani Morogoro.

Ujenzi huo unaohusisha njia ya msongo wa Kilovoti 33 kutokea kituo kidogo cha Zuzu hadi Mbande wenye thamani ya Sh5.1 bilioni.